MCT YATANGAZA WATEULE 18 WA TUZO ZA EJAT, WASHINDI KUTANGAZWA MEI 29 DAR


DAR ES SALAAM. 

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesisitiza Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) zimejikita zaidi katika kutambua thamani ya taaluma, weledi na athari za kazi za waandishi wa habari badala ya kuangalia fedha au umaarufu wa mshiriki.

Hayo yameelezwa leo Mei 19, 2026 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti,kamati ya Maandalizi ya EJAT, Ernest Sungura wakati wa kutangaza wateule 18 wa EJAT msimu wa 16 waliopatikana kupitia mfumo mpya wa kidigitali uliotumika kwa mara ya kwanza kuchakata kazi 594 za waandishi wa habari katika makundi 11 ya tuzo hizo.

Sungura Amesema kuwa utofauti wa EJAT na tuzo nyingine unatokana na kuheshimu misingi ya taaluma ya uandishi wa habari na kuweka mkazo katika umahiri, ushahidi wa athari za habari kwa jamii pamoja na matumizi ya viwango vya kitaaluma katika tathmini.

Kupitia mfumo huo mpya, kazi 60 ziliondolewa mapema kwa kukosa vigezo vya msingi kabla ya kufikishwa kwa majaji huku tathmini ikifanyika bila upendeleo kwa kuwa alama pekee ndizo zilizotumika kufanya maamuzi.

Aidha, MCT imesema baada ya kutangazwa kwa washindi, mfumo huo utafunguliwa kwa washiriki wote waliojiandikisha ili kuwawezesha kuona maeneo yaliyowakwamisha na namna wanavyoweza kujiboresha zaidi katika kazi zao za uandishi wa habari.

Katika mkutano huo, Baraza la Habari Tanzania pia limeitangaza Taasisi ya Uwezo Tanzania kuwa mshirika wake muhimu katika utekelezaji wa tuzo hizo kupitia programu maalum ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika eneo la elimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Uwezo Tanzania Baraka Mgohamwende amesema taasisi hiyo tayari imeanza fellowship maalum ya uandishi wa habari za elimu inayolenga kuwawezesha waandishi kutumia tafiti na tathmini mbalimbali katika kuandaa habari zenye umahiri na zenye kuleta matokeo kwa jamii.

Ameongeza kuwa fellowship hiyo itakuwa ikifanyika kwa kipindi cha miezi sita ambapo waandishi watapatiwa mafunzo pamoja na uwezeshaji wa kufanya kazi kwa vitendo katika kuandaa habari za kitaaluma.

Kwa mujibu wa Uwezo Tanzania, awamu ya kwanza ya programu hiyo ilianza na waandishi 17 lakini waandishi 12 pekee ndio waliofanikiwa kuendelea na programu.

Katika hatua nyingine, EJAT imetangaza kuwa washindi wa msimu wa 16 watatajwa rasmi Mei 29, 2026 katika ukumbi wa Four Points By Sheraton (New Africa), Dar es Salaam, ambapo Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera atakuwa mgeni rasmi.

Wateule 18 waliotangazwa ni pamoja na Shaban Hamisi wa Nipashe, Simon Mkina wa Pambazuko Online, Daniel Samson wa Nukta Africa, Devotha Kihwelo wa Mwananchi, Abdallah Kurwa wa ITV pamoja na Joseph Kirati wa The Chanzo na wengine.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.