Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala jijini Dar es Salaam limefanikiwa kuopoa miili miwili iliyokuwa inaelea majini katika maeneo ya Stakishari, Ukonga na daraja la Sarenda, na kisha kuikabidhi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Zimamoto Duniani, Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Ilala, SACF Mabusi Peter, alisema tukio la kwanza lilihusisha mwili wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60, uliopolewa jana jioni katika eneo la Stakishari, Ukonga.
Amesema mwili mwingine wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 21 hadi 26 uliopolewa leo majira ya saa tano asubuhi katika daraja la Sarenda, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi waliouona ukielea majini.
“Leo asubuhi tukiwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja tulipokea taarifa ya kuwepo kwa mwili wa mwanaume usiyefahamika ukielea katika daraja la Sarenda. Tulifika eneo la tukio na kuufanyia uokoaji. Vilevile, jana tuliopoa mwili wa mwanamke katika eneo la Stakishari. Miili yote tumekabidhi kwa vyombo husika kwa uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Mabusi.
Aidha, Kamanda Mabusi ametoa wito kwa wananchi kuwa makini katika kipindi hiki cha mvua kinachoendelea, akisisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari wanapovuka mito na maeneo yenye maji mengi ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo.


Hakuna maoni: