MVUA DAR: TARURA YATOA MAELEKEZO KWA MAKANDARASI


Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam umesema kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara unaendelea katika maeneo yote yasiyoathirika moja kwa moja na mvua hizo.

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Mei 10, 2026, TARURA imeeleza kuwa kazi zinazoendelea ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya DMDP II na CERC, ikiwemo ujenzi wa mifereji, makaravati, barabara za zege pamoja na maandalizi mengine ya kiufundi katika maeneo mbalimbali ya miradi.

Aidha, wakala huo umesema umewaelekeza makandarasi wote kuhakikisha wanaimarisha na kutunza njia mbadala ili ziweze kupitika wakati wote hata kipindi cha mvua kubwa, kwa lengo la kuepusha kufungwa kwa barabara, msongamano wa magari pamoja na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa makandarasi wametakiwa kuhakikisha njia hizo mbadala zinakuwa na mifumo madhubuti ya kupitisha maji ya mvua ili kuzuia uharibifu na kurahisisha magari kupita kwa usalama.

Sambamba na hilo, makandarasi wameagizwa kuweka vibao vya tahadhari, alama elekezi za usalama pamoja na taa za usiku katika maeneo yote ya kazi ili kuwaongoza watumiaji wa barabara na kuongeza usalama kipindi hiki cha mvua zinazoendelea.

Pia TARURA imesisitiza umuhimu wa makandarasi kuendelea kufuata kikamilifu programu za kazi zilizokubaliwa kimkataba ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora unaotakiwa ndani ya muda uliopangwa.

Katika hatua nyingine, wakala huo umeeleza kuwa unaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi hiyo ili kuhakikisha miundombinu inayotekelezwa inakamilika kwa ubora na manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

TARURA imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na kufuata maelekezo yanayotolewa katika maeneo yote ya miradi kwa ajili ya usalama wao pamoja na kurahisisha utekelezaji wa kazi hizo.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.