Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Asemewe Taifa, Geofrey Kiliba, ametoa wito kwa vijana nchini kujiepusha na vitendo au mienendo inayoweza kuhatarisha maslahi yao pamoja na kuathiri amani ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kiliba amesema vijana wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa, hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya upotoshaji unaoweza kuwafanya wachukue hatua zisizo sahihi.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda amani akieleza kuwa maendeleo ya nchi yanategemea utulivu uliopo, na kwamba jitihada zozote za kuuvuruga hazipaswi kuungwa mkono.
“Maendeleo ya taifa letu yanahitaji mshikamano na ulinzi wa amani; vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vyote vinavyoweza kuleta vurugu,” amesema.
Aidha, alibainisha kuwa kuna watu wachache wanaotumia mbinu za kushawishi na kupotosha ili kuwavuta vijana katika mwelekeo usiofaa, hali ambayo inaweza kuleta athari kubwa kwa mustakabali wao.
Alionya kuwa iwapo amani ya nchi itayumba, vijana ndio watakaobeba mzigo mkubwa wa athari hizo, hivyo ni muhimu kuwa na msimamo thabiti katika kulinda taifa.
Kiliba pia aliwataka vijana kuepuka kuburuzwa katika ajenda za kisiasa zisizo na manufaa, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu mifumo ya uongozi iliyopo kwa mujibu wa Katiba.
Katika kuimarisha maendeleo ya vijana, alizitaka taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi stadi kuhakikisha zinaboresha huduma zao ili kuwajengea vijana ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Vilevile, alieleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa vijana kupitia utoaji wa mikopo kwa vikundi mbalimbali, ambapo mamia ya vikundi tayari vimepata fursa hiyo.
Alitaja pia kuanzishwa kwa wizara inayoshughulikia maendeleo ya vijana chini ya Ofisi ya Rais kuwa ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya Serikali katika kuwainua vijana.
Kiliba aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 na programu nyingine zinazolenga kuwawezesha kiuchumi.
Kwa upande mwingine, alisema yuko tayari kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha vijana kunufaika na fursa hizo kwa kusambaza taarifa sahihi na kuondoa upotoshaji uliopo katika jamii.
Aliongeza kuwa juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ni kielelezo cha namna inavyotambua mchango wa vijana na dhamira yake ya kuhakikisha wanakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.

Hakuna maoni: