Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Chama cha NCCR-Mageuzi kimemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Avaline Wilbard Munisi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo, Mei 7, 2026 Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Faustin Sungura, chama hicho kimesema uteuzi huo ni heshima kubwa kwa chama pamoja na uthibitisho wa imani iliyopo kwa viongozi wake.
Sungura amesema kuwa Dkt. Munisi awali aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuteuliwa tena kuwa Naibu Waziri katika serikali ya awamu ya sita.
NCCR-Mageuzi kimesema kuwa pamoja na malengo mengine ya chama hicho, moja ya dhamira yake kuu ni kushika dola kwa njia ya halali na kidemokrasia, huku kikieleza kuwa nguvu ya chama hutokana na kuwa na viongozi pamoja na wanachama bora.
“Chama chetu ni chama pekee ambacho kutokana na ubora wa viongozi wake, kimeaminiwa na mwanachama wetu kukabidhiwa nafasi ya unaibu waziri, jambo ambalo ni kubwa na la kujivunia,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, chama hicho kimewataka baadhi ya watu wanaokikosoa chama hicho kuacha kutumia maneno ya kejeli dhidi ya Dkt. Munisi na badala yake kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ya kitaifa.
Katika taarifa hiyo, NCCR-Mageuzi pia kimemhakikishia Dkt. Munisi kuwa kitaendelea kumpa ushirikiano wa karibu ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwatumikia wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mwisho, chama hicho kimemtakia afya njema na mafanikio katika kazi zake mpya huku kikisisitiza kuwa uteuzi huo ni ishara ya kuthamini mchango wa chama hicho katika siasa na maendeleo ya nchi.



Hakuna maoni: