Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Ngome ya Vijana Taifa ya Chama cha ACT Wazalendo imesema mfumo uliotumika kusimamia na kutoa mikopo ya vijana yenye thamani ya shilingi bilioni 200 umeacha maswali mengi kuhusu uwazi, usawa na namna fedha hizo zinavyowafikia walengwa nchini.
Akizungumza Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome hiyo, Abdul Nondo alisema chama hicho kilipinga tangu mwanzo uamuzi wa Serikali kusambaza fedha hizo kupitia wizara za kisekta badala ya kuwa chini ya mfumo mmoja wa uratibu wa vijana.
Amesema hali hiyo imechangia kuwepo kwa changamoto za uwajibikaji na ukosefu wa taarifa za kina kuhusu mchakato mzima wa utoaji wa mikopo hiyo.
“Mpaka sasa hakuna taarifa za kutosha kuhusu walionufaika au namna fedha hizo zinavyotolewa kupitia wizara mbalimbali,” alisema Nondo.
Pia ACT Wazalendo ilikosoa masharti yaliyowekwa kwa vijana waliotaka kuomba mikopo hiyo, ikiwemo hitaji la kuwa na leseni ya biashara pamoja na vigezo vingine walivyodai vinawakwamisha vijana wengi.
Chama hicho pia kilieleza kutoridhishwa na muda wa siku 12 uliotolewa kwa ajili ya maombi ya mikopo hiyo, kikidai haukutosha kuwafikia vijana wengi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, jumla ya vijana 30,384 pekee waliwasilisha maombi ya mikopo hiyo.



Hakuna maoni: