Na Mwandishi Wetu,
Jeshi la Polisi Wilaya ya Mbogwe kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limetoa mafunzo ya ukamataji salama kwa maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Hifadhi ya Msitu wa Taifa Kigosi, yakilenga kuongeza weledi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi.
Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika Mei 8, 2026 katika Makao Makuu ya Hifadhi ya Kigosi yaliyopo Iponya, wilayani Mbogwe mkoani Geita, yakihusisha askari kutoka kambi mbalimbali za hifadhi hiyo.
Akitoa mafunzo hayo, Kamanda wa Operesheni wa Polisi Wilaya ya Mbogwe, SP T.I Kilakoi, aliwataka askari wa uhifadhi kuzingatia matumizi sahihi ya nguvu wakati wa ukamataji ili kuepusha madhara yasiyo ya lazima.
Alisema askari wanapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya silaha za moto, ikiwamo kutambua mazingira yanayoruhusu matumizi ya silaha hizo wakati wa operesheni.
“Mtuhumiwa anapokamatwa lazima apewe haki zake za msingi, ahojiwe kwa wakati na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi,” alisema SP Kilakoi.
Aidha, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuthamini ushirikiano uliopo kati yake na TFS katika kukabiliana na uhalifu ndani ya hifadhi, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano huo kupitia operesheni za pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Kigosi, PCO Jared Otieno, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa kuwajengea uwezo maafisa na askari wa uhifadhi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Otieno alimshukuru SP Kilakoi kwa kuitikia mwaliko wa TFS na kutoa mafunzo yaliyogusa masuala muhimu ya ukamataji, matumizi ya nguvu na ushughulikiaji wa vielelezo.
Alisema TFS itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa mafunzo ya mara kwa mara, huku ikipanga kupanua wigo wa washiriki kwa kuwajumuisha askari kutoka vituo vya TFS vilivyopo wilaya zinazopakana na Hifadhi ya Kigosi.



Hakuna maoni: