Dodoma
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mheshimiwa Emily Burns katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo katika jengo la Tume ya Madini, Kilimani Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mavunde alibainisha kuwa moja ya kipaumbele kikuu cha sekta ya madini ni utafiti ambao utapelekea kutambua aina na kiwango cha rasilimali madini tulizobarikiwa nchini kwetu na kuvutia uwekezaji.
"Tunafamu kuwa Nchi yetu tumeweza kufanya utafiti wa kina wa kurusha ndege kwa asilimia 16 tu. Hivyo, tuna uhitaji mkubwa wa kupata uwekezaji zaidi katika eneo hili ili kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye maendeleo ya Nchi yetu"
"Na ndiyo maana Nchi yetu tumeigawa katika bloku 6, ambapo mpaka sasa bloku moja pekee ipo mbioni kuanza kufanyiwa utafiti kupitia mradi unatakaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia Serikali ya Spain. Bado kuna fursa kubwa ya wawekezaji wengine katika bloku 5 zilizobaki" alisisitiza Mhe. Mavunde.
Vilevile, Serikali chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira wezeshi yanayovutia uwekezaji, hivyo nitoe rai kwa wadau na kampuni kutoka nchini Canada kuja kuchangamka fursa ya kuwekeza kwenye sekta ya madini nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Burns aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano inaotoa kwake na kueleza utayari wa Kampuni kutoka nchini Canada kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Aidha, Mheshimiwa Burns alieleza kuwa amefurahishwa na namna Tanzania tunavyosimamia shughuli za uchimbaji mdogo na kusisitiza kuwa Canada ipo tayari kuyaleta makampuni ya utengenezaji wa vifaa vya uchimbaji hususan uchenjuaji madini ili viweze kusaidia kuongeza tija kwa wachimbaji wadogo nchini.








Hakuna maoni: