SONGWE
Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Biashara (Joint Trade Committee – JTC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia umeanza leo tarehe 4 Mei 2026 mjini Tunduma mkoani Songwe, kujadili masuala ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ikiwemo uondoshwaji wa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru vinavyowakabili wafanyabiashara wa nchi hizo mbili wakati wa kuvuka mpaka.
Mkutano huo wa siku nne kuanzia tarehe 4 hadi 7 Mei 2026 umeanza katika ngazi ya Wataalamu ambapo wanajadili na kuanda ajenda zitakazowasilishwa kwa Makatibu Wakuu watakaokutana tarehe 6 Mei 2026, kabla ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika Mei 7, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, katika ngazi ya Wataalamu Mkurugenzi wa Mtangamo wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara - Tanzania Bw. Ombeni Mwasha amesisitiza kuhusu umuhimu wa majadiliano ya uwazi na kina ili kupata suluhisho la kudumu dhidi ya changamoto zinazoathiri ustawi wa sekta ya biashara kati ya pande hizo mbili.
“Mkutano huu ni muendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina yetu. Tunakumbuka waasisi wetu walivyoshirikiana kuondoa ukoloni; sasa ni wajibu wetu kushirikiana kutumia ipasavyo fursa za kiuchumi zilizopo kwa maendeleo ya nchi zetu na kuboresha maisha ya wananchi.” alisema Bw. Mwasha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa katika Wizara ya Biashara na Viwanda - Zambia na mwenyekiti mwenza wa mkutano huo Dkt. Simon Ng’ona ameeleza kuhusu utayari wa Nchi hiyo wa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutatua changamoto zilizopo, akibainisha kuwa hatua hiyo itarahisisha na kuongeza mwingiliano wa bidhaa, huduma na watu, pamoja na kuchangia ukuaji wa maendeleo ya uchumi wa kanda.
Mkutano wa JTC pamoja na muasula mengine unalenga kuunganisha juhudi za pamoja katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia, kwa kujadili na katatua changamoto mbalimbali ikiwemo maboresho ya sera, kurahisisha taratibu za forodha, na kuendeleza miundombinu ya kimkakati ili kuongeza kiwango cha biashara, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya mataifa hayo mawili na ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).








Hakuna maoni: