TANZANIA YATAKA MSIMAMO WA PAMOJA KULINDA SOKO LA ALMASI ASILIA

Freetown, nchini Sierra Leone

Tanzania imezitaka nchi Wanachama Zinazozalisha Almasi Afrika (ADPA) kuweka msimamo wa pamoja katika kulinda soko la almasi asilia dhidi ya ongezeko la almasi zinazotengenezwa maabara ambazo zimeendelea kuathiri thamani na uaminifu wa soko la madini hayo duniani.

Wito huo ulitolewa Mei 20, 2026 na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa ADPA uliofanyika mjini Freetown, nchini Sierra Leone, ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya almasi Barani Afrika pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hiyo duniani.

Dkt. Kiruswa alisema umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya mawasiliano na masoko ili kuongeza uelewa kwa walaji kuhusu tofauti kati ya almasi asilia na almasi zinazotengenezwa maabara sambamba na kulinda uhalisia, thamani na mchango wa almasi asilia katika uchumi wa nchi zinazozalisha madini hayo.

Vilevile, alisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana ili kuwa na mikakati ya pamoja ya kuhakikisha madini yanaongezwa thamani ndani ya bara la Afrika ili kupata manufaa zaidi kutokana na uwepo wa rasilimali hizo katika nchi za Afrika.

Mkutano huo ulipitisha mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuimarisha matumizi sahihi ya sifa za kimataifa zitakazotofautisha wazi almasi asilia na zile za sintetiki, pamoja na kuhamasisha taasisi za kimataifa za biashara ya almasi kuunga mkono juhudi hizo kwa manufaa ya sekta ya almasi barani Afrika.

Aidha, nchi hizo zilikubaliana kuimarisha umoja huo ili kukabiliana na changamoto za Biashara ya Almasi duniani.


#InvestInTanzania #MIningSector

#MineralForGrowth

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.