Tabora, Mei 21, 2026
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umewataka wananchi wanaojihusisha na ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yatokanayo na nyuki kuzingatia viwango vya ubora na usalama wa bidhaa zao, ukionya kuwa uzalishaji usiozingatia sheria unaweza kuhatarisha masoko ya ndani na nje ya nchi.
Tahadhari hiyo ilitolewa leo na Meneja wa Rasilimali Nyuki wa TFS, SACC Hussein Msuya, wakati wa majadiliano ya biashara kwa biashara na mdahalo kuhusu maendeleo ya sekta ya ufugaji nyuki nchini, uliofanyika katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Vita mkoani Tabora kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani.
SACC Msuya alisema Tanzania imeendelea kujijengea sifa kimataifa kutokana na ubora wa mazao yake ya nyuki, hususan asali na nta, lakini akasisitiza kuwa ubora huo unaweza kupotea iwapo wafugaji na wachakataji hawatazingatia viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
“Utumiaji wa vifungashi bora ni takwa la kisheria na unasimamiwa na sheria ya viwango. Kwa mujibu wa kanuni za ufugaji nyuki, asali lazima ifungashwe kwa ubora na iwekwe lebo kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya ufugaji wa nyuki,” alisema SACC Msuya.
Alisema baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni pamoja na matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango, uchakataji usiozingatia usafi pamoja na uhifadhi usiofaa wa bidhaa za nyuki, hali inayoweza kushusha ubora wa bidhaa na kupunguza imani ya wanunuzi.
Aidha, aliwataka wananchi kutumia vifaa sahihi wakati wa uvunaji na uchakataji wa asali, nta na gundi ya nyuki ili kuhakikisha bidhaa hizo zinadumu katika ubora unaokubalika kwenye soko la ushindani.
“Wito wangu kwa wananchi ni kujikita katika matumizi ya vifungashio vilivyoidhinishwa na vinavyokidhi viwango vya ubora na usalama wa asali,” alisisitiza.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mdahalo huo waliishukuru TFS kwa kuendelea kutoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki, wakisema mafunzo hayo yatawawezesha kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na kuongeza kipato cha kaya zao.
Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yanaendelea katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Vita mkoani Tabora, huku wananchi wakihamasishwa kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ili kujifunza teknolojia za kisasa za ufugaji nyuki na kushiriki kilele cha maadhimisho hayo kitakachofanyika kesho Mei 22, 2026.







Hakuna maoni: