TFS YATOA VIFAA VYA TEHAMA KWA SHULE YA JUHUDI JESHINI

Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki imetoa msaada wa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya Sh milioni 6.3 kwa Shule ya Sekondari Juhudi Jeshini ya Gongolamboto, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, mashine ya fotokopi, printer na kabati la kuhifadhia nyaraka.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, Mathew Ntilicha, Mhifadhi Mkuu James Kabuta alisema msaada huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia huku TFS ikiendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na misitu ya asili.

Kabuta alisema TFS itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira na kuwataka kuacha uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti ovyo, badala yake washiriki katika upandaji miti na utunzaji wa mazingira.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Sakina Omary, alisema msaada huo utasaidia kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji, akibainisha kuwa shule ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa vifaa vya TEHAMA.

“Vifaa hivi vitawasaidia walimu kufundisha kwa urahisi zaidi na wanafunzi kupata nafasi ya kujifunza TEHAMA kwa vitendo,” alisema Sakina.

Naye Dada Mkuu wa shule hiyo, Angel Palsivo, alisema wanafunzi watanufaika kwa kupata maarifa ya kisasa ya teknolojia huku wakiahidi kuvitunza vifaa hivyo kwa manufaa ya wanafunzi wa sasa na baadaye.

Aidha, Angel alisema shule hiyo ina klabu ya mazingira inayohamasisha wanafunzi kushiriki katika shughuli za upandaji miti na usafi wa mazingira.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.