Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa msimu wa Kipupwe wa Juni hadi Agosti mwaka 2026 unatarajiwa kuwa na hali ya baridi katika maeneo mengi ya nchi, huku mwezi Julai ukitajwa kuwa na vipindi vya baridi kali zaidi.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya mwenendo wa hali ya hewa kwa kipindi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kusini pamoja na Nyanda za Juu Kusini-Magharibi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi.
Aidha, amesema maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini na kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani, huku baadhi ya maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuka hadi chini ya nyuzi joto 10 za sentigredi.
Dkt. Chang’a amesema msimu huo pia utatawaliwa na upepo kutoka Kusini Mashariki wenye nguvu iliyopungua kidogo, lakini kutakuwepo vipindi vya upepo mkali zaidi katika miezi ya Juni na Julai hususan kwenye maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya nchi kavu.
Kwa upande wa mvua, TMA imeeleza kuwa licha ya msimu wa Kipupwe kwa kawaida kuwa wa ukavu, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za nje ya msimu, ikiwemo Kanda ya Ziwa Victoria hususan Mkoa wa Mara pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha, TMA imeonya kuwa hali ya baridi na vumbi inaweza kuongeza magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji kama mafua na homa ya mapafu, pamoja na magonjwa ya macho na yale yanayoathiri mifugo.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imezitaka jamii, wakulima, wafugaji pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa pamoja na tahadhari zinazotolewa ili kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli zao za kila siku.





Hakuna maoni: