Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), wamezindua rasmi Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha elimu ya hali ya hewa, tahadhari za mapema pamoja na usalama majini nchini.
Uzinduzi huo umefanyika Mei 28, 2026 katika ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam ambapo wadau mbalimbali wa habari na mazingira walihudhuria.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Uchechemuzi kutoka EMEDO, Bi. Mary Francis Mahemba, alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuielimisha jamii kuhusu madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa, tahadhari za mapema na namna ya kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.
Alisema kupitia tuzo hizo, wanahabari watapata nafasi ya kutambuliwa kwa kazi zao zinazosaidia kuokoa maisha ya wananchi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu hali ya hewa na usalama majini.
“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga,” alisema Bi. Mahemba.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo zitalenga habari zinazohusu matukio ya hali mbaya ya hewa, tahadhari za mapema, usalama wa usafiri wa majini, uzuiaji wa ajali za kuzama maji pamoja na ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayotokana na hali ya hewa.
Aidha, Meneja Masoko na Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni, alisema matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa yana mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi, hasa wale wanaotegemea shughuli za maji kama uvuvi na usafiri wa majini.
Alisema TMA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanahabari wanatambuliwa kwa mchango wao katika kuelimisha jamii kuhusu masuala ya hali ya hewa nchini.
Waandishi wa habari kutoka redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali wamealikwa kushiriki kwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani kuanzia Agosti 1, 2025 hadi Agosti 30, 2026.


Hakuna maoni: