TUME YA TAIFA YA MIPANGO YASISITIZA TAFITI NA UBUNIFU ZA ARU ZIJIELEKEZE KUINUA UCHUMI WA KISASA TANZANIA
Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia masuala ya Biashara na Ubunifu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango Dkt. Blandina Kilama amesisitiza kuwa maendeleo endelevu ya nchi yanategemea kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika tafiti na bunifu zitakaosaidia kutatua changamoto za wananchi ikiwa ni utekelezaji wa dira ya maendeleo 2050.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa wiki ya tafiti na bunifu za Chuo Kikuu Ardhi iliyofanyika chuoni hapo leo 18 Mei, 2026 Dkt. Kilama amebainisha kuwa Chuo Kikuu Ardhi kimeendelea kuwa kinara katika kuzalisha tafiti na bunifu zinazochochea maendeleo hapa nchini, jambo linalofanya ARU kuwa kiungo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Tunastahili kuwapongeza kwa kuwa vinara wa kubadilisha nadharia kuwa vitendo. Tafiti zinatakiwa kubadilika kuwa biashara, na ARU imeweza kuonyesha hilo kwa vitendo," amesema Dkt. Kilama.
Katika hotuba yake, kiongozi huyo alieleza kuwa Tanzania hivi sasa inahitaji kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na kuwa Tume ya Taifa ya Mipango inafarijika kuona tafiti zinazofanywa na wataalamu nchini zinatumika moja kwa moja kutatua matatizo halisi yanayowakabili wananchi.
Dkt. Kilama ametoa wito maalum kwa watafiti na wanafunzi wa ARU kutumia kikamilifu fursa wanazozipata chuoni hapo ili kuonyesha uwezo na kutoa michango yao ya kiubunifu huku akiongeza kuwa mazingira bora ya ubunifu yanastawi pale ambapo watu wenye taaluma na ujuzi tofauti wanapokutana na kushirikiana kwa pamoja.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Evaristo Liwa, ameeleza kuwa chuo hicho kinawaandaa wanafunzi kwa vitendo ili kuwawezesha kutumia elimu yao katika kutatua changamoto za kijamii na kujipatia kipato, hatua ambayo imewajengea kujiamini na kuwasaidia kuanzisha kampuni binafsi, kufanya tafiti, pamoja na kubuni masuluhisho ya kudumu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya ardhi majenzi.
Wiki ya maonesho ya tafiti na bunifu ya Chuo Kikuu Ardhi iliyobeba kauli mbiu ya “Mageuzi ya maarifa ya kitaaluma suluhisho la kibiashara: Bunifu sekta ya Ardhi na Majenzi”
Imefunguliwa jana tarehe 18 Mei 2026 na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22 Mei 2026.
Katika wiki hii wanafunzi na wanataaluma wataendelea kuonesha tafiti na bunifu zao kwa jamii na wakati huo huo wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi watakuwa wakitoa huduma kupitia kliniki maalum ya ardhi (Ardhi Kliniki) yenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali katika masuala ya ardhi na kutoa huduma za utoaji wa hati miliki.a

Hakuna maoni: