WAFANYAKAZI TARURA WAHIMIZWA KUENDELEA KUFANYA KAZI KWA UFANISI LICHA YA MAFANIKIO



‎Tabora.

‎Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, amewataka wafanyakazi wa Wakala huo kuendelea kuongeza juhudi, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao licha ya pongezi wanazoendelea kupokea kutoka kwa wananchi kutokana na maboresho ya miundombinu nchini.

‎Mhandisi Seff ametoa rai hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TARURA uliofanyika mkoani Tabora, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii zaidi katika kuwahudumia wananchi.

‎"Tunapokea pongezi nyingi kutoka kwa wananchi kutokana na kazi nzuri inayofanywa na TARURA lakini mafanikio hayo yasitufanye turidhike. Tunapaswa kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuongeza juhudi ili kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi", amesema Mhandisi Seff.

‎Ameongeza kuwa anatambua mchango mkubwa wa watumishi wa TARURA nchini kote, akibainisha kuwa jitihada zao zimekuwa na manufaa makubwa tangu kuanzishwa kwa Wakala huo kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara za vijijini na mijini.

‎Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TAMICO) Bw. Paternus Rwechungura, ameipongeza TARURA kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na wafanyakazi kupitia mikutano ya Baraza la Wafanyakazi.

‎Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Bi. Happyness Makombe, amepongeza juhudi za watumishi wa TARURA kwa kujituma katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara nchini.

‎Amesema mafanikio ya TARURA yanaonekana wazi kupitia kuongezeka kwa upatikanaji wa barabara zinazopitika wakati wote hali inayorahisisha usafirishaji wa mazao, utoaji wa huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi.

‎Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Bw. Tamsoni Mshighati, amewapongeza watumishi wa TARURA kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

‎Aidha, amewahimiza wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuendelea kuimarisha ustawi wa watumishi pamoja na hadhi ya mabaraza ya wafanyakazi nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.