Na Mwandishi Wetu.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Uhusiano, Deus Sangu, amezindua Bodi ya Saba ya Ushauri ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Katika uzinduzi huo uliofanyika leo, Waziri Sangu amesema Bodi hiyo ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu kwa OSHA ili kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo na kuhakikisha mikakati inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuzingatia dira, dhima na malengo ya Serikali.
Amesema miongoni mwa majukumu ya Bodi ni kushauri uandaaji na utekelezaji wa mpango mkakati wa OSHA, kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi kupitia taarifa za mwaka na hesabu za Wakala, pamoja na kutoa ushauri kuhusu maslahi na stahili za watumishi ili kuongeza motisha, uwajibikaji na tija mahali pa kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameielekeza Bodi kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 155 na 187 ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vya usalama na afya mahali pa kazi vinaendelea kuzingatiwa nchini.
Aidha, ameitaka Bodi kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kidijitali ukiwamo mfumo wa Workplace Information Management System (WIMS), kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi na wadau.
“Majukumu haya yatekelezwe kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali pamoja na misingi ya uwajibikaji, uadilifu, ubunifu, ushirikiano kazini na uwazi,” amesema Waziri Sangu.
Sambamba na hilo, amesema Bodi inaanza majukumu katika kipindi muhimu ambapo Serikali inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, huku uzinduzi wa Mpango Mkakati wa OSHA ukiwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi.
Waziri Sangu pia ameisisitiza Bodi kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo iliyowekwa huku akiitaka kutoa nafasi kwa Menejimenti ya OSHA kusimamia shughuli za kila siku bila kuingiliwa.
Amesema jukumu kuu la Bodi ni kutoa ushauri na usimamizi wa kimkakati ili kuhakikisha kila upande unatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri OSHA, Makwaia Makani, ameishukuru Serikali kwa imani iliyowaonesha na kuahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.
Awali akizungumza, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema bodi zina mchango mkubwa katika maendeleo ya taasisi hiyo na Menejimenti iko tayari kushirikiana na Bodi mpya kuendelea kuimarisha utendaji na utoaji huduma.



Hakuna maoni: