WCF YATAKA WANAHABARI KUWA MABALOZI WA ELIMU YA FIDIA KWA WAFANYAKAZI

 


Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema waandishi wa habari nchini wanapaswa kutumia taaluma na vyombo vyao vya habari kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma zinazotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na kuhamasisha wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi.

Nyamhokya amesema hayo leo Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kuhusu fidia kwa wafanyakazi kwa wanachama wa Chama cha Waandishi Wanaofanya Kazi Katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) yaliyoandaliwa kwa ushirikiano na WCF.

Amesema mafunzo hayo yatawawezesha waandishi wa habari kupata uelewa wa masuala ya fidia kwa wafanyakazi na kuwa katika nafasi nzuri ya kuhabarisha umma kwa usahihi kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo.

“Waandishi wa habari ni daraja muhimu la kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali. Tunatarajia mkimaliza mafunzo haya mtakuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha waajiri kujisajili WCF na kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati,” amesema Nyamhokya.

Pia amesema WCF ni taasisi muhimu kwa wafanyakazi kwani imeanzishwa kushughulikia fidia kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi wanaopata ajali, magonjwa au vifo vinavyotokana na kazi.

Amesema mafao yanayotolewa na WCF ni pamoja na huduma za matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na kudumu, malipo kwa wategemezi wa mfanyakazi aliyefariki, huduma za utengemao pamoja na msaada wa mazishi.

Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa na wataalam wa WCF ili waweze kueneza elimu hiyo kwa jamii na maeneo yao ya kazi.

Sambamba na hilo, Nyamhokya amesema mshikamano wa wafanyakazi ni silaha muhimu katika kutetea haki na maslahi yao kupitia kauli mbiu ya “Solidarity Forever.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma Siwayombe amesema mafunzo hayo yataimarisha mahusiano kati ya WCF, vyama vya wafanyakazi na vyombo vya habari.

Pia ameishukuru WCF chini ya uongozi wa John Mduma kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa wanachama wa JOWUTA kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

“Tunashukuru sana uongozi wa WCF kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hii kwa wanahabari. Tunaamini huu ni mwanzo wa mafunzo kama haya kufanyika katika kanda nyingine nchini,” amesema Siwayombe.

Aidha, amesema wanahabari wanapaswa kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa jamii kwa kueleza umuhimu wa WCF katika kulinda ustawi wa wafanyakazi wanaopata madhara, majeraha, magonjwa au vifo vitokanavyo na kazi zao.

Siwayombe amesema bado wanahabari wengi nchini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa ajira za kudumu na mikataba ya kazi jambo linalowakosesha haki mbalimbali ikiwemo kunufaika na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Pia amewasihi wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasajili wanahabari katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na mfuko huo.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kushughulikia changamoto za wanahabari nchini kwa kuchukua hatua dhidi ya waajiri wanaowatumia wanahabari bila ajira rasmi wala mikataba ya kazi.

Aidha mshikamano na umoja ni muhimu kwa wafanyakazi katika kudai haki zao kupitia kaulimbiu ya wafanyakazi duniani ya “Solidarity Forever.”

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.