WCF YAWAHIMIZA WAJIRI KUJISAJILI NA KUWASILISHA MICHANGO KWA WAKATI

Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umewataka waajiri wote katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara kuhakikisha wanajisajili na kuwasilisha michango kwa wakati kwa mujibu wa sheria ili kuwawezesha wafanyakazi kupata haki zao wanapopatwa na madhara yatokanayo na kazi.

Hayo yameelezwa na Afisa wa WCF Ayoub Bendera wakati akiwasilisha mada kuhusu Usajili na Michango katika mafunzo kwa wanahabari wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) yaliyofanyika Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kwa lengo la kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi wanazozifanya.

Aidha amesema waajiri wote katika sekta rasmi wanatakiwa kuchangia asilimia 0.5 ya mapato ya mfanyakazi kila mwezi ambapo michango hiyo ni jukumu la mwajiri na hairuhusiwi kukatwa kwenye mshahara wa mfanyakazi.

“Usajili katika Mfuko ni takwa la kisheria na unafanyika bure kupitia mfumo wa mtandaoni wa WCF ambapo mwajiri anaweza kujaza taarifa za taasisi, kuwasilisha viambatisho muhimu na kupata cheti cha usajili bila kufika ofisini,” amesema.

Amevitaja baadhi ya viambatisho vinavyotakiwa wakati wa usajili kuwa ni cheti cha TIN, leseni ya biashara, cheti cha usajili wa taasisi pamoja na taarifa za mishahara ya wafanyakazi (Payroll).

Pia amesema michango yote huwasilishwa kwa njia ya kielektroniki kupitia mfumo wa WCF ePG kwa kutumia namba maalum ya malipo (Control Number), huku waajiri wakitakiwa kuwasilisha michango ndani ya muda uliopangwa na sheria.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.