Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limebaini kuwa Ramadhan Jafari maarufu kama Muna (47), ambaye aliripotiwa kupotea hivi karibuni, aliuawa na kufukiwa ndani ya nyumba yake iliyopo Mbezi Luguruni Kwembe, Wilaya ya Ubungo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema hii leo Juni 23, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema Juni 16, 2026 ndugu wa karibu wa marehemu walitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kimara Gogoni kuhusu kupotea kwake. Baada ya kupokea taarifa hiyo, Polisi waliinza uchunguzi na ufuatiliaji kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vitengo mbalimbali vya kiusalama.
Uchunguzi uliofanyika baadaye ulibaini kuwa Ramadhan Jafari alikuwa ameuawa na mwili wake kufukiwa ndani ya moja ya vyumba vya nyumba yake. Polisi waligundua kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo ni mtoto wa marehemu, Juma Ramadhan maarufu kama Juli (21), ambaye alikamatwa katika eneo la Msufini, Msoga mkoani Pwani.
Baada ya kukamatwa, mtuhumiwa alidai kueleza namna alivyotekeleza mauaji hayo na kisha kuchimba shimo ndani ya nyumba kabla ya kuufukia mwili wa baba yake. Hata hivyo, Polisi wamesema sababu zilizomsukuma kufanya kitendo hicho bado zinaendelea kuchunguzwa.
Jeshi la Polisi limelaani vikali tukio hilo na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kutoa taarifa za uhalifu. Polisi pia wameonya kuwa watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu watachukuliwa hatua kali za kisheria mara ushahidi utakapokamilika.

Hakuna maoni: