MIRADI YA TAA KUKUZA UTALII,BIASHARA NA UWEKEZAJI



Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege nchini unalenga kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye katika sekta ya usafiri wa anga.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TAA, Irene Minja, ambaye amesema mamlaka hiyo imejizatiti kuendelea kuzingatia uwajibikaji, uwazi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yake, sambamba na kusimamia miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Minja amesema uwekezaji unaoendelea kufanywa katika sekta ya viwanja vya ndege una mchango mkubwa katika kukuza biashara, utalii na uwekezaji, huku viwanja hivyo vikiendelea kuwa lango muhimu la kuiunganisha Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

“Tunatambua nafasi ya viwanja vya ndege katika maendeleo ya nchi, ndiyo maana tunaendelea kuboresha huduma na miundombinu ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kivutio cha watalii, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia,” amesema Minja.

Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia TAA, kujifunza kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.