DODOMA.
Waziri wa Nishati, Mhe.Deogratius Ndejembi, amesema Serikali imejipanga kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 4,300 za sasa hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa ya uzalishaji wa umeme nchini.
Amesema hayo akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma
Akifafanua kuhusu hilo amesema kuwa, Dira ya Taifa imeweka lengo la kufikia uzalishaji wa megawati 74,000 za umeme ifikapo mwaka 2050, huku maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi yakielekeza Taifa kufikia angalau megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Mhe.Ndejembi amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Nishati imeweka mikakati madhubuti ya kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme itakayosaidia kufikia lengo hilo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua wa megawati 100 katika eneo la Kishapu mkoani Shinyanga, ambao aliutaja kuwa wa kihistoria kutokana na ukubwa wake.
Amssema tayari megawati 50 zimeanza kupatikana kupitia mradi huo na kwamba uzalishaji wa megawati zote 100 unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Ndejembi pia ametangaza kuanza kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawati 2,000 kwa kutumia makaa ya mawe katika eneo la Mchuchuma wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Amesema licha ya Tanzania kuwa na hifadhi kubwa ya makaa ya mawe, bado nchi haijaanza kuzalisha umeme kupitia rasilimali hiyo, jambo ambalo Serikali sasa inalikwenda kulibadilisha kupitia mradi huo mkubwa.
“Taifa letu lina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe lakini hatuzalishi hata megawati moja kwa kutumia makaa ya mawe. Sasa tunaanza utekelezaji wa mradi huu wa megawati 2,000 katika eneo la Mchuchuma,” amesema
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya uzalishaji wa umeme kupitia gesi asilia kwa kutekeleza mradi wa Kinyerezi III ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 1,000 na kuziingiza katika Gridi ya Taifa.
Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Kakono wenye uwezo wa kuzalisha megawati 87 pamoja na Mradi wa Malagarasi ambao unaendelea na utekelezaji wake.
Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini, kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na kusaidia Tanzania kufikia malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



Hakuna maoni: