BODI YA KOROSHO TANZANIA YAKABIDHI VIUATILIFU VYA THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 1.9 KWA WAKULIMA WA BONDE LA KILOMBERO

Na: Daud Moses Mbanile - Ifakara TC

Bodi ya Korosho Tanzania leo Juni 17, 2026 imekabidhi viuatilifu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kwa wakulima wa zao la korosho katika Bonde la Kilombero, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao hilo.

Akizungumza katika hafla ya mapokezi iliyofanyika katika ghala la Ifakara AMCOS, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Dkt. Yuda Mgeni, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe .Wakili Dunstan Kyobya amesema kuwa wamepokea viuatilifu vya korosho kutoka Bodi ya Korosho ambavyo vimekabidhiwa UKICU, jumla ya lita 15,843 zimekabidhiwa kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima wa korosho waliosajiliwa kwenye mfumo, ambapo Halmashauri ya Mji Ifakara imepatiwa lita 339, Mlimba lita 1,606, Ulanga lita 8,037 na Malinyi lita 5,858. Aidha, ameeleza kuwa viuatilifu hivyo vitagawiwa kwa wakulima wa korosho waliosajiliwa kwenye mfumo ili kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo katika Bonde la Kilombero.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Mkoa wa Morogoro, Bw. Jafari Matata amewataka wakulima kujisajili kwa haraka ili waweze kunufaika na ruzuku hiyo ya viuatilifu vinavyotolewa bure, huku akisisitiza kuwa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu hivyo itaendelea kutolewa ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuwezesha Mkoa wa Morogoro kufikia lengo la kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa zao la korosho nchini.

Naye Mwenyekiti wa UKICU, Bi. Ritha Nyera amesema wataendelea kuwahamasisha wakulima kujikita zaidi katika uzalishaji wa zao la korosho ili kuboresha ubora wa mazao na kuongeza ushindani wake katika soko la ndani na nje ya nchi, sambamba na kufikia malengo ya kuuza korosho zenye viwango vya juu vya ubora.

Mmoja wa wakulima, Bw. Gwakisha Emmanuel ameishukuri Serikali kwa viuatilifu hivyo kwani vitaongeza tija ya uzalishaji wa korosho katika Bonde la Kilombero, kwani hapo awali wakulima walikabiliwa na changamoto ya wadudu pamoja na uzalishaji mdogo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.