Na Agnes Njaala,
Itamboleo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Brigedia Jenerali Maulid Surumbu, ameongoza zoezi la upandaji miti katika maeneo yaliyopitiwa na Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Tanzania–Zambia (TAZA), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha uoto wa asili na kulinda vyanzo vya maji vinavyochangia uzalishaji wa umeme nchini.
Zoezi hilo limezinduliwa Juni 11, 2026 katika Shule ya Msingi Majombe, Kijiji cha Itamboleo wilayani Mbarali, ambapo miti zaidi ya 200 imepandwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Brigedia Jenerali Surumbu alisema maeneo yenye mikondo ya maji yanayoelekea kwenye mito inayolisha mabwawa ya kuzalisha umeme yanapaswa kupewa kipaumbele katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.
“Tunawapongeza TANESCO kupitia Mradi wa TAZA kwa kuanzisha mpango huu wa kurejesha uoto wa asili ulioathiriwa wakati wa utekelezaji wa mradi. Hii ni hatua muhimu inayounganisha maendeleo ya miundombinu na uhifadhi wa mazingira,” alisema.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mazingira wa Mradi wa TAZA, Mhandisi Fikirini Mtandika, aliyemwakilisha Meneja wa Mazingira wa TANESCO, Bw. Tluway Sappa, alisema uzinduzi huo ni sehemu ya mpango wa urejeshaji mazingira unaotekelezwa katika vijiji 22 vya Wilaya ya Mbarali vilivyopitiwa na mradi huo.
Alisema TANESCO imepanga kupanda zaidi ya miti 2,000 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, hususan karibu na vyanzo vya maji vinavyochangia mtiririko wa Mto Ruaha Mkuu, ambao ni muhimu kwa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera, Kidatu na Julius Nyerere.
“Tunatambua umuhimu wa mazingira katika kulinda vyanzo vya maji vinavyosaidia uzalishaji wa umeme. Ndiyo maana tunaendelea kutekeleza programu za upandaji miti katika maeneo mbalimbali yanayozunguka miradi yetu,” alisema Mhandisi Mtandika.
Naye Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Mbarali kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Lucas Bitta Bwire, alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi wanaozunguka misitu ya Chimala na Ulembo pamoja na maeneo yaliyopitiwa na Mradi wa TAZA.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za uhifadhi na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha juhudi za kulinda mazingira zinafanikiwa na kuleta manufaa endelevu kwa jamii na taifa kwa ujumla.






Hakuna maoni: