Dar es Salaam
Chama cha Madereva wa Masafa Marefu Tanzania kimekanusha taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii zikidai kuwa madereva wanajiandaa kufanya mgomo katika siku za hivi karibuni, kikieleza kuwa hakuna mpango wowote wa kusitisha shughuli za usafirishaji nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Dede, amesema madereva wa masafa marefu wanaendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida na hawana nia ya kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuvuruga shughuli za kiuchumi au kudhoofisha juhudi za Serikali za kukuza uchumi wa taifa.
Amesema sekta ya usafirishaji ni mhimili muhimu wa maendeleo ya nchi, hivyo madereva wana wajibu wa kuhakikisha huduma za usafirishaji zinaendelea kutolewa kwa ufanisi ili kuchochea biashara, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.
“Tunatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na usafirishaji. Hatuko tayari kushiriki katika jambo lolote litakalovuruga juhudi hizo au kuathiri ustawi wa uchumi wa nchi yetu,” amesema Dede.
Aidha, amesema chama hicho kinaendelea kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu ya usafirishaji na mazingira ya uwekezaji.
Kuhusu taarifa za mgomo zinazoenezwa na baadhi ya makundi kupitia mitandao ya kijamii, Dede amesema chama chake hakijahusishwa kwa namna yoyote na mipango hiyo wala hakijatoa wito wa mgomo kwa wanachama wake.
Pia amewataka madereva wote nchini kuendelea kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za nchi, huku wakijiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na utulivu wa taifa.
Amesisitiza kuwa amani na utulivu ni nguzo muhimu za maendeleo ya taifa, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika hatua nyingine, Dede amewataka madereva wa malori na mabasi kutoshiriki maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika Julai 7, akieleza kuwa chama hicho kinaamini masuala yote yanaweza kutatuliwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa, huku kikiendelea kutanguliza amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.

Hakuna maoni: