






Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa tuzo kwa waajiri 11 waliofanya vizuri katika kuwasilisha taarifa na kusimamia urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa waajiriwa wao, hatua inayolenga kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mikopo hiyo kutoka kwa wanufaika.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema urejeshaji wa mikopo ni takwa la kisheria na kwamba waajiri wanapaswa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wapya ndani ya siku 15 tangu kuajiriwa kwao ili kuwezesha utekelezaji wa marejesho ya mikopo wanayodaiwa.
Amesema HESLB inatambua mchango mkubwa wa taasisi zinazozingatia sheria ya urejeshaji wa mikopo, ndiyo sababu imeamua kuzitunuku taasisi hizo ili kuongeza hamasa kwa waajiri wengine kufuata mfano huo.
“Kupitia waajiri hawa 11, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mikopo. Fedha zinazorejeshwa zinasaidia kutimiza ndoto za vijana wengine wanaohitaji kupata elimu ya juu,” amesema Dkt. Kiwia.
Ameongeza kuwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hali inayoongeza mahitaji ya mikopo, hivyo urejeshaji wa mikopo kwa wakati ni muhimu ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, kiwango cha ukusanyaji wa mikopo kimeendelea kuongezeka kila mwaka, ambapo HESLB ilikusanya Sh bilioni 169 mwaka 2022, Sh bilioni 177 mwaka 2023 na Sh bilioni 194.5 katika mwaka wa fedha 2024/2025. Bodi hiyo inalenga kukusanya Sh bilioni 220 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema ili kuongeza ufanisi wa urejeshaji wa mikopo, HESLB imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayorahisisha uhifadhi wa taarifa na ukusanyaji wa madeni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kurejesha mikopo.
“Wapo watu wanaoamini wanaweza kukwepa kulipa deni hili, nawasisitiza kuwa huu si msaada wa bure bali ni mkopo unaopaswa kurejeshwa. Tunakamilisha mfumo wa kisasa unaotumia teknolojia ya akili mnemba (AI) ambao utasaidia kuwafikia wadaiwa popote walipo,” amesema.
Aidha, amesema HESLB inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa kimkakati wakiwemo NSSF, Posta, TRA, RITA, NIDA na TCU katika kuhakikisha urejeshaji wa mikopo unakuwa wenye tija zaidi.
Dkt. Kiwia amesema tuzo zilizotolewa ni ishara ya kuthamini uzalendo na ushirikiano wa waajiri wanaotekeleza wajibu wao kwa maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa taasisi zilizotunukiwa tuzo hizo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya NMB, Black Tanzania Limited, Benki ya CRDB, Benki ya NBC, Tanzania Empowerment Limited, Vodacom Tanzania, Hospitali ya Shifaa na Mohamed Enterprises Limited.
Kwa upande wake, Naibu Meneja wa Rasilimali Watu wa TRA, Tija Opondwa, ameishukuru HESLB kwa kutambua mchango wa waajiri wanaotekeleza wajibu wao wa kusimamia urejeshaji wa mikopo, akisema mamlaka hiyo inachukulia suala hilo kwa uzito mkubwa.
Amesema utoaji wa tuzo hizo utakuwa chachu kwa taasisi nyingine kuongeza juhudi katika kutekeleza wajibu huo muhimu.
Naye mwakilishi wa Hospitali ya Shifaa, Sahil Ratif, amesema taasisi hiyo itaendelea kuzingatia weledi na ubora katika utoaji wa huduma zake huku ikihakikisha inatimiza wajibu wake wa kushirikiana na HESLB katika urejeshaji wa mikopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukopeshaji na Urejeshaji Mikopo wa HESLB amesema waajiri wanaoshirikiana na bodi hiyo hujiepusha na adhabu na faini zinazotokana na kutowasilisha au kutorejesha makato ya mikopo kwa wakati.
“Waajiri hawatoi fedha kutoka mifukoni mwao, bali hukata makato hayo kwenye mishahara ya waajiriwa wanaodaiwa. Kutekeleza wajibu huu kwa wakati kunawasaidia kuepuka faini zisizo za lazima,” amesema.

Hakuna maoni: