KIGOMA.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro (IGP Mstaafu), leo tarehe Juni 18, 2026 ametangaza kuwa Mkoa wa Kigoma uko tayari kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yatakayofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25 Juni 2026, yakihusisha wadau wa sekta ya usafiri majini kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na nchi jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Sirro alisema maadhimisho hayo yameratibiwa na Wizara zenye dhamana ya uchukuzi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma pamoja na wadau wa sekta ya usafiri majini.
Alisema kwa kipindi cha siku nne za maadhimisho kutakuwa na maonesho ya huduma za taasisi mbalimbali, utoaji wa elimu kuhusu usalama wa usafiri majini, kampeni za matumizi salama ya vyombo vya majini, warsha za kitaalamu, shughuli za kijamii na maonesho ya uokoaji wakati wa dharura.
Mhe. Sirro alisema uzinduzi rasmi wa maadhimisho utafanyika tarehe 22 Juni 2026 ukiongozwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Mohamed, huku kilele chake kikifanyika tarehe 25 Juni 2026 chini ya Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb.).
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika kuboresha usafiri wa majini mkoani Kigoma kupitia ukarabati wa Bandari ya Kigoma, maboresho ya meli ya MV Liemba, ujenzi wa meli mpya pamoja na kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji majini kwa uwepo wa Boti ya Uokoaji ya TASAC II.
Akihitimisha, Mhe. Sirro amewataka wananchi wa Kigoma na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo na kuviomba vyombo vya habari kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa tukio hilo la kitaifa.





Hakuna maoni: