KILIMO IKOLOJIA CHAPANUA FURSA KUPITIA TEKNOLOJIA YA UONGEZAJI THAMANI

WAZALISHAJI 20 WA KILIMO IKOLOJIA WANOLEWA TEKNOLOJIA YA KUONGEZA THAMANI MAZAO

Morogoro.

Wazalishaji 20 wa mazao ya kilimo ikolojia kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wamepatiwa mafunzo ya teknolojia za kuongeza thamani ya mazao kupitia ziara ya kujifunza iliyofanyika katika Kiwanda cha Intermech mkoani Morogoro.

Ziara hiyo iliratibiwa na Shirika la Island of Peace (IDP) kwa kushirikiana na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA) chini ya Mradi wa ECO-FOOD unaolenga kuimarisha mifumo endelevu ya chakula.

Washiriki walipata fursa ya kujifunza matumizi ya mashine mbalimbali za uchakataji wa mazao, hatua inayolenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuboresha ubora wa bidhaa, kuimarisha vifungashio na kuongeza muda wa kuhifadhi bidhaa sokoni.

Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, washiriki walisema teknolojia walizojifunza zimewapa hamasa ya kuendeleza kilimo ikolojia na kuwekeza zaidi katika uchakataji wa mazao ili kuongeza thamani na kipato.

Aidha, walieleza kuwa uwekezaji katika teknolojia za uchakataji unafungua fursa mpya za masoko na ajira huku ukichangia ujenzi wa mfumo wa chakula endelevu na wenye tija kwa jamii.

Mradi wa ECO-FOOD unatekelezwa kwa ushirikiano wa IDP na MVIWAARUSHA ukiwa na lengo la kuwawezesha wakulima na wajasiriamali katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya kilimo ikolojia kupitia mafunzo, kubadilishana uzoefu na kujengewa uwezo wa kibiashara.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.