Dar es Salaam.
Jukwaa la Vijana Taifa la Chama cha Ukombozi wa Umma (JUVICHA) limesema vijana nchini bado wanakabiliwa na mazingira magumu ya kiuchumi licha ya kuwa nguzo muhimu katika uzalishaji na maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 24, 2026 katika Makao Makuu ya CHAUMA yaliyopo Kinondoni Biafra jijini Dar es Salaam, Mratibu wa JUVICHA Taifa, Masoud Mambo, alisema vijana ndio kundi kubwa linaloguswa na maamuzi yanayofanywa na Serikali, lakini mchango wao haujawekewa mazingira stahiki ya kuwawezesha kufanikiwa kiuchumi.
Mambo alisema changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana zimeendelea kuongezeka kutokana na uwepo wa sheria, sera na taratibu ambazo kwa kiasi kikubwa zinawazuia kupata fursa za ushindani katika soko la ndani na la kimataifa.
Alieleza kuwa tatizo la ukosefu wa ajira linaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wengi, huku idadi kubwa ya wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka wakilazimika kujiajiri katika sekta zisizo rasmi kutokana na nafasi chache zilizopo katika sekta rasmi.
Kwa mujibu wa takwimu za Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana, alisema kati ya vijana milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, asilimia 20 pekee hupata ajira rasmi, huku asilimia 80 wakijikita katika shughuli za uchumi zisizo rasmi kama biashara ndogondogo na usafirishaji wa bodaboda.
Aidha, JUVICHA imekosoa hatua ya Serikali kuongeza gharama za usajili wa baadhi ya vyombo vya usafiri ikiwemo bodaboda, ikidai kuwa hatua hiyo inaongeza mzigo kwa vijana wengi wanaotegemea sekta hiyo kujipatia kipato.
Mambo pia alidai kuwa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 haijatoa majibu ya kudumu kwa changamoto za ajira kwa vijana, akisema mikopo inayotolewa kwa makundi maalumu haiwezi kuwa suluhisho la kudumu bila kuwepo kwa mazingira bora ya uwekezaji na uzalishaji.
Wakati huo huo, JUVICHA imetangaza kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yatakayofanyika Agosti 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Mambo alisema jukwaa hilo litaadhimisha siku hiyo chini ya kaulimbiu isemayo, “Vijana, Wakati ni Sasa”, yenye lengo la kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wao na taifa kwa ujumla.
Alisema maadhimisho hayo yatatoa fursa ya kujadili mchango wa vijana katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi pamoja na kuhimiza ushiriki wao katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya nchi.

Hakuna maoni: