Dar es Salaam, Juni 8, 2026.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani vitendo vya kukamatwa na kushikiliwa kwa wananchi kinyume cha sheria katika maeneo mbalimbali nchini, huku kikizitaka mamlaka husika kuhakikisha haki za kisheria za wanaoshikiliwa zinalindwa.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo, LHRC imesema imepokea malalamiko ya wananchi kushikiliwa kwa muda mrefu bila dhamana au kufikishwa mahakamani katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Shinyanga, Morogoro na Singida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zaidi ya wananchi 200 wa Kata ya Idukilo wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, wanadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa muda mrefu kwa makosa yanayostahili dhamana. Aidha, LHRC imesema imepokea taarifa za madai ya vipigo pamoja na uharibifu wa nyumba na maduka ya baadhi ya wananchi katika eneo hilo.
Vilevile, wananchi wanne wa Kijiji cha Njiwa wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, wanadaiwa kuendelea kushikiliwa tangu Juni 3, 2026 bila dhamana wala kufikishwa mahakamani, huku watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wakidaiwa kushikiliwa kwa zaidi ya siku nane bila kufikishwa mahakamani.
Kutokana na hali hiyo, LHRC imezitaka mamlaka za polisi katika maeneo husika kuwaachia kwa dhamana wanaostahili dhamana au kuwafikisha mahakamani bila kuchelewa ikiwa kuna tuhuma zinazowakabili.
Pia, taasisi hiyo imewataka viongozi wa Serikali na vyombo vya dola kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na kufuata taratibu za kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
LHRC imesema itaendelea kufuatilia kwa karibu matukio hayo na kuchukua hatua stahiki za kisheria ili kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Hakuna maoni: