MAONESHO YA VYUO VIKUU VYA MALAYSIA YAVUTA MAMIA DAR ES SALAAM

DAR ES SALAAM. 

Mamia ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wamejitokeza kushiriki maonesho ya vyuo vikuu bora kutoka Malaysia yaliyofanyika katika Hoteli ya Serena, yakilenga kutoa fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Tanzania.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea maonesho hayo yaliyofanyika Juni 3, washiriki mbalimbali walisema maonesho hayo yamefungua milango ya maarifa na kuwapa vijana nafasi ya kufahamu fursa za masomo zinazopatikana katika vyuo vikuu vya kimataifa.

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Warda Masud, alisema maonesho hayo yamemhamasisha kuendelea na masomo ya uzamili nchini Malaysia kutokana na ubora wa vyuo vyake, ambavyo baadhi yake vimeorodheshwa miongoni mwa vyuo 50 bora duniani.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema tukio hilo limechangia kukuza soko la elimu nchini kwa kuwaunganisha vijana wa Kitanzania na taasisi za elimu zenye viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko kutoka Education Malaysia Global Services (EMGS), Esther Low, alisema lengo la ujio wao nchini ni kuwahamasisha vijana wa Tanzania kutumia fursa za elimu zinazotolewa na vyuo vikuu vya Malaysia pamoja na kujenga ushirikiano na taasisi za elimu za Tanzania.

Kabla ya kufanyika kwa maonesho hayo, viongozi wa Global Education Link na EMGS walifanya mazungumzo na viongozi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wadau wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa elimu ya juu kati ya Tanzania na Malaysia kupitia kubadilishana wanafunzi na wataalamu, kuendeleza tafiti za pamoja na kuongeza fursa za elimu ya kimataifa kwa wanafunzi wa Kitanzania.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano ya kielimu kati ya Tanzania na Malaysia na kuweka mazingira bora yatakayowezesha vijana wa Tanzania kupata elimu yenye viwango vya kimataifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.