Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, leo Juni 27, 2026 ameshiriki Mbio za Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking Marathon) zilizofanyika katika Viwanja vya St. Peters Oysterbay jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza wakati wa kufungua mbio hizo, Mhe. Salome amesema pamoja na hatua nzuri iliyofikiwa, matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini bado yako katika kiwango cha asilimia 28.6, hali inayoonesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kufikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amesema mbio hizo si mashindano ya kawaida ya kutafuta medali au vikombe, bali ni chachu ya mabadiliko ya kifikra na kijamii yanayolenga kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuwawezesha wananchi kiuchumi, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Ameongeza kuwa mafanikio ya lengo hilo yanahitaji ushiriki wa Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa Tanzania ina kila sababu ya kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika matumizi ya nishati safi ya kupikia iwapo ushirikiano utaendelea kuimarishwa.
Aidha, amebainisha kuwa tukio hilo ni sehemu ya kuthamini na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Mhe. Salome ameeleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wa Dar es Salaam katika marathon hiyo, pia amewashukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA) kwa kuandaa tukio hilo muhimu na wadau mbalimbali waliofanikisha tukio hilo wakiwemo Taasisi za Serikali, kampuni za nishati safi ya kupikia, vyombo vya habari pamoja na wanamichezo walioshiriki mbio hizo.
Kupitia marathon hiyo ametoa wito kwa wananchi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, vijana kuwa mabalozi wa mabadiliko hayo kupitia teknolojia na mitandao ya kijamii, na pia amewahamasisha Mama Lishe na Baba Lishe kutumia nishati safi ili kulinda afya zao, afya za wateja wao na kupunguza gharama za uendeshaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, Mjiolojia Mkuu, Bw. Ngereja Mgejwa, amesema marathoni hiyo ni moja ya mbinu zinazotumiwa kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwani matumizi ya michezo yamekuwa njia bora ya kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja na kuwawezesha kuelewa faida za nishati safi katika kulinda afya, mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Naye, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA), Bi. Noreen Mawalla, amewashukuru wadhamini, washiriki na wadau wote waliofanikisha Nishati Safi Expo 2026 pamoja na Clean Cooking Marathon, akisema lengo la kampeni hiyo ni kufikisha elimu na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi katika mikoa mbalimbali nchini.
Amebainisha kuwa kampeni hiyo imefikia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha.
Amesema kampeni inaendelea kuifikia mikoa mingine sita katika kila kanda ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata uelewa kuhusu manufaa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Washindi wa Mbio za Kitaifa za Nishati Safi ya Kupikia walizawadiwa mitungi ya gesi na majiko banifu kama sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.








Hakuna maoni: