MRADI WA SH2.5 BILIONI WA UTALII MAGAMBA WAPANDISHA HADHI YA TFS KUELEKEA AFCON 2027

 


Na Mwandishi Wetu, 

Lushoto Tanga.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Magamba Eco Forest Lodge Ltd, mradi wa utalii wa ikolojia wenye thamani ya Sh2.5 bilioni unaotarajiwa kuifanya Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini na kuongeza uwezo wa Tanzania kupokea wageni kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Mradi huo unaowekezwa na Harmeet Grewal ulizinduliwa Juni 26, 2026 wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea wilaya ya Lushoto kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiambatana na pongezi kwa juhudi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuendeleza utalii unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba, Joyce Kabuchi, alisema mradi huo utagharimu Sh2.5 bilioni, huku zaidi ya Sh1.5 bilioni tayari zikiwa zimewekezwa katika hatua za awali za utekelezaji.

Alisema ujenzi wa lodge hiyo ya kisasa utaongeza thamani ya vivutio vya utalii vilivyopo katika Milima ya Usambara, kuongeza muda wa watalii kukaa eneo hilo, kuchochea ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta ya utalii.

“Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Magamba kuwa kitovu cha utalii wa ikolojia nchini, sambamba na kuhamasisha uhifadhi endelevu wa misitu na mazingira,” alisema Kabuchi.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wazo Michael Mwang’onda, aliipongeza TFS kwa kuendelea kuvutia wawekezaji katika maeneo ya hifadhi, akisema miradi hiyo inaonyesha namna uhifadhi wa mazingira unavyoweza kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.

Mbali na kuweka jiwe la msingi wa Magamba Eco Forest Lodge, Mwenge wa Uhuru ulifungua eneo la uwekezaji wa utalii wa ikolojia la Grewal, linalosimamiwa na TFS, na kupongeza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuendeleza utalii endelevu.

Katika ziara hiyo, Mwenge wa Uhuru pia ulizindua matanki ya maji katika Kijiji cha Gologolo. Ilielezwa kuwa vyanzo vya maji hayo vinatoka katika hifadhi zinazohifadhiwa na TFS, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa kulinda misitu na vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu ya wananchi.

TFS pia iligawa miche zaidi ya 100 ya miti kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa upandaji miti, uhifadhi wa misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Lushoto yaliwashirikisha watumishi wa TFS kutoka Ofisi ya Meneja wa Misitu wa Wilaya (DFC) Lushoto, Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba, Shamba la Miti Shume na Kurugenzi ya Mbegu, pamoja na viongozi wa wilaya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Lushoto, na wabunge wa majimbo ya Mlalo na Bumbuli.

Uwekezaji wa Magamba Eco Forest Lodge ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuimarisha utalii wa ikolojia nchini kupitia uboreshaji wa miundombinu ya malazi, huduma na vivutio vya utalii. Mkakati huo unalenga kuiwezesha Tanzania kunufaika na ongezeko la watalii wa ndani na nje ya nchi, hususan wakati wa AFCON 2027, ambapo nchi itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa ushirikiano na Kenya na Uganda.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.