MRADI WA MTO MKUJU-RUVUMA KUCHANGIA ASILIMIA 4 YA URANI DUNIANI

 


Namtumbo, Ruvuma

Mradi wa Urani wa Mto Mkuju uliopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya urani duniani, huku ukikadiriwa kuchangia takribani asilimia 4 ya uzalishaji wa urani duniani mara utakapofikia hatua ya uzalishaji.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo mapema wiki hii, Meneja wa Mradi wa Mto Mkuju, Beria Vorster, alisema maandalizi ya utekelezaji wa mradi yanaendelea kwa kasi na kwamba mradi huo una umuhimu mkubwa katika kukidhi mahitaji ya nishati safi duniani.

“Mradi wa Mto Mkuju ni miongoni mwa miradi mikubwa ya urani barani Afrika. Uzalishaji utakapoanza, unatarajiwa kuchangia takribani asilimia 4 ya uzalishaji wa urani duniani, jambo ambalo litaiweka Tanzania katika nafasi muhimu kwenye soko la kimataifa la madini hayo,” alisema Vorster.

Kwa mujibu wa Shirika la World Nuclear Association (WNA), mwaka 2024 uzalishaji wa urani duniani uliongozwa na Kazakhstan kwa asilimia 39, ikifuatiwa na Canada kwa asilimia 24 na Namibia kwa asilimia 12. Uzbekistan ilichangia takribani asilimia 7, huku Urusi ikichangia kati ya asilimia 4 hadi 5 ya uzalishaji wa dunia. Hivyo, makadirio ya Mradi wa Mto Mkuju kuchangia asilimia 4 ya uzalishaji wa urani duniani yanaweza kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa uzalishaji wa urani duniani mara mradi huo utakapoanza uzalishaji wa kibiashara.

Alifafanua kuwa urani itakayozalishwa nchini Tanzania haitahusishwa kwa namna yoyote na utengenezaji wa silaha za nyuklia, bali itatumika kuzalisha nishati safi inayotumika katika vituo vya kuzalisha umeme wa nyuklia duniani.

Vorster alisema Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (Treaty on the Non-Proliferation of Nuclear Weapons - NPT), hali inayoweka misingi madhubuti ya kuhakikisha matumizi ya madini ya urani yanazingatia malengo ya amani na maendeleo endelevu.

“Urani kutoka Tanzania itatumika katika uzalishaji wa nishati safi na salama. Serikali ya Tanzania pamoja na taasisi za kimataifa zina mifumo madhubuti ya usimamizi na ufuatiliaji kuhakikisha madini haya yanatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa pekee,” alisisitiza Vorster.

Aliongeza kuwa katika kipindi ambacho dunia inaelekea kwenye matumizi ya nishati zenye kiwango kidogo cha uzalishaji wa hewa ukaa, nishati ya nyuklia imeendelea kupewa kipaumbele kama sehemu ya suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi na mahitaji ya umeme yanayoongezeka.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo kwa wananchi, Meneja wa Mradi wa Mto Mkuju, Beria Vorster, alisema mradi unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,000 za moja kwa moja pindi utakapoanza shughuli zake za uzalishaji kwa kiwango kamili, sambamba na maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja kupitia utoaji wa huduma kwenye mradi.

Alisema Kampuni imeanza mapema kuandaa rasilimali watu kutoka maeneo yanayouzunguka mradi ili kuhakikisha wananchi wa eneo husika wanakuwa sehemu ya mafanikio ya mradi huo.

“Tayari vijana 100 kutoka vijiji vinavyozunguka mradi wameshapatiwa mafunzo ya uendeshaji wa mitambo mbalimbali inayotumika katika shughuli za uchimbaji na usindikaji wa madini. Kati yao, vijana 10 tayari wameajiriwa na mradi, na programu hii itaendelea ili kuandaa wataalamu zaidi watakaohitajika wakati wa utekelezaji kamili wa mradi,” alisema Vorster.

Aliongeza kuwa mkakati huo unalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mradi na kuhakikisha ujuzi na teknolojia vinahamishiwa kwa wananchi wa maeneo husika.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Eng. Alphonce Bikulamchi, alisema pamoja na ajira za moja kwa moja, mradi huo utafungua mamia ya fursa nyingine katika sekta za usafirishaji, huduma za chakula, biashara, ujenzi, malazi na huduma nyingine zinazohusiana na shughuli za uchimbaji madini.

“Mradi huu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma. Mbali na mapato yatakayopatikana kwa Serikali, wananchi watanufaika kupitia ajira, ongezeko la shughuli za kiuchumi na ukuaji wa biashara zinazozunguka mradi,” alisema Eng. Bikulamchi.

Kwa kuzingatia ukubwa wa akiba zake, mchango wake katika uzalishaji wa urani duniani, pamoja na fursa za ajira na uwekezaji zitakazozalishwa, Mradi wa Mto Mkuju unatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati inayoweza kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa madini ya urani kwa matumizi ya nishati safi duniani.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.