OFISI YA DKT. KIKWETE YAKANUSHA KUHUSIKA NA MPANGO WA UWEKEZAJI MTANDAONI

 OFISI YA DKT. KIKWETE YAKANUSHA TUHUMA ZA KUHUSISHWA NA MPANGO WA UWEKEZAJI WA AI

Ofisi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, imekanusha taarifa zinazosambazwa mtandaoni zikidai kuwa kiongozi huyo anahusishwa na mpango wa uwekezaji unaotumia Akili Unde (AI) na kuwaahidi Watanzania kupata mapato makubwa baada ya kuwekeza fedha.

Katika taarifa yake kwa umma, Ofisi hiyo imesema madai yanayodai kuwa maelfu ya Watanzania wamepata mafanikio kupitia uwekezaji wa Shilingi 653,000 na kupata zaidi ya Shilingi milioni 9.2 kwa mwezi ni ya uongo na yanalenga kuwapotosha wananchi.

Ofisi hiyo imeeleza kuwa Dkt. Kikwete hajawahi kuhusika, kuidhinisha, kutangaza wala kuunga mkono mpango wowote wa aina hiyo. Pia imesisitiza kuwa haijatoa ruhusa ya matumizi ya jina, picha au hadhi ya Rais huyo Mstaafu katika kutangaza shughuli zozote zinazohusiana na uwekezaji huo unaodaiwa kuwepo.

Aidha, wananchi wamehimizwa kuwa waangalifu dhidi ya matapeli wanaotumia majina ya viongozi na watu maarufu kuwavutia watu kujiunga na mifumo isiyo halali ya uwekezaji.

Ofisi ya Dkt. Kikwete imewataka wananchi kupuuza taarifa hizo na kuepuka kujisajili, kutuma fedha au kusambaza ujumbe wowote unaohusiana na mpango huo, ikieleza kuwa ni habari za uongo zisizo na ukweli wowote.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.