Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ni nyenzo muhimu katika kuleta mageuzi ya sekta ya afya nchini Tanzania.
Amesema ushirikiano huo una nafasi kubwa katika kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma bora za afya pamoja na kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 6, jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la PPP kuhusu Mageuzi ya Sekta ya Afya chini ya FYDP IV na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, lililofanyika katika Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS). Kongamano hilo liliwakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa afya na wawekezaji kujadili fursa za kuimarisha ushirikiano wa PPP katika sekta ya afya
Kafulila amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo uwekezaji uliowezesha baadhi ya matibabu maalumu yaliyokuwa yakifanyika nje ya nchi kupatikana ndani ya Tanzania.
Ameeleza kuwa ongezeko la idadi ya watu, kuongezeka kwa umri wa kuishi na mahitaji makubwa ya huduma za afya za kibingwa vinaifanya serikali kushindwa kugharamia mahitaji yote ya sekta hiyo kwa kutumia mapato ya kodi na mikopo pekee.
“Uchumi wetu unaendelea kukua na mahitaji ya huduma za afya yanaendelea kuongezeka. Uwezo wa serikali kugharamia huduma zote hizi kwa kutumia kodi na mikopo una mipaka,” amesema Kafulila.
Kwa upande wake, Rais wa Medical Association of Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo akisema wadau wanapaswa kubaini maeneo ambayo sekta binafsi inaweza kuleta ubunifu na kuboresha huduma ambazo bado hazipatikani au zinazotolewa kwa kiwango kisichoridhisha.
Amehimiza wawekezaji na wataalamu wa afya kujifunza kutoka kwa mifano ya mafanikio ya mataifa mengine na kuangalia namna bora ya kuitumia katika mfumo wa afya wa Tanzania.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Association of Private Health Facilities in Tanzania (APHFTA), Dk Mahmood Mringo, amesema PPP haipaswi kuonekana kama uhamishaji wa mtaji kutoka sekta binafsi kwenda sekta ya umma pekee, bali kama njia ya kuhamasisha rasilimali zote zilizopo kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi.
Amesema afya na elimu ni huduma muhimu za msingi zinazohitaji mifumo endelevu ya ufadhili pamoja na ubia wa kibunifu ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Dk Mringo amebainisha kuwa wananchi huchangia maendeleo ya taifa kupitia kodi na hivyo wanastahili kupata huduma bora za afya zinazokidhi matarajio yao.








Hakuna maoni: