PUTIN AAHIDI FURSA ZAIDI KWA TANZANIA

Na Beda Msimbe, TBC, Moscow

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi yake itaendelea kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji kwa Tanzania kwa manufaa ya pande zote mbili.

Putin amesema Urusi kwa sasa ina miradi zaidi ya 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imechangia kutoa ajira zaidi ya 3,018. Aidha, amesema fursa zaidi zitatangazwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi utakaofanyika nchini Urusi kesho kutwa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Putin alisema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi yanayoendelea nchini Tanzania na kuridhishwa na kasi ya maendeleo yanayopatikana.

Alisema mazungumzo yao yamekuwa yenye tija na manufaa makubwa kwa wananchi wa mataifa yote mawili, huku akiahidi kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi.

Kwa upande wake, Rais Samia alisema ziara yake nchini Urusi ina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwake binafsi na kwa Taifa la Tanzania, ikizingatiwa kuwa ni zaidi ya miaka 50 imepita tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini humo.

"Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Hivyo, kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu," alisema Rais Samia.

Rais Samia pia alikumbusha mchango mkubwa wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kumpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.

Rais Samia yuko nchini Urusi kwa ziara yake ya kwanza katika taifa hilo, ambayo pia ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa Tanzania nchini humo katika kipindi cha zaidi ya nusu karne.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi, pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.