Na Beda Msimbe, TBN, Moscow
Kengele kubwa iliyogongwa mara tisa huku bendi ya jeshi ikiongoza nyimbo za maombolezo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, majira ya saa tano na dakika 23 leo aliweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyefahamika mjini Moscow, Urusi.
Baada ya shughuli hiyo, iliyofanyika katika eneo ambalo moto huwaka daima kama kumbukumbu ya wapiganaji wa Urusi waliopoteza maisha katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, vikosi vitatu vya gwaride vilipita kwa mwendo wa heshima mbele ya Rais Samia huku wimbo wa Taifa wa Tanzania ukipigwa.
Nidhamu ya hali ya juu iliyooneshwa na askari waliokuwa wakilinda eneo hilo, waliosimama bila kutikisika katika nafasi zao, pamoja na utaratibu wa kubadilishana zamu za ulinzi na mwendo wa taratibu uliomsindikiza Rais Samia hadi eneo la kumbukumbu, vilikuwa miongoni mwa mambo yaliyovutia wengi waliohudhuria hafla hiyo.
Baadaye, Rais Samia, ambaye yuko nchini Urusi kwa ziara ya kiserikali, alikutana na mwenyeji wake, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kwa mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Katika ushirikiano wa kijeshi uliopo kati ya Tanzania na Urusi, zaidi ya maofisa 300 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamepata nafasi za masomo ya shahada ya kwanza na ya pili nchini Urusi.
Maofisa hao wamekuwa wakipatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya ugaidi, sayansi na teknolojia, mafunzo ya kijeshi, operesheni za kulinda amani, ununuzi na uhifadhi wa silaha pamoja na mbinu za kukabiliana na majanga.
Tanzania na Urusi zinaendeleza ushirikiano wa kijeshi kwa kuzingatia makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi yaliyosainiwa mwaka 2016 na makubaliano ya ushirikiano wa kiufundi wa kijeshi yaliyotiwa saini mwaka 2018.
Kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania uliokuwa asilimia 5.5 mwaka 2024 na makadirio ya kufikia asilimia 6 mwaka huu, pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ziara ya Rais Samia nchini Urusi inatarajiwa kuimarisha fursa za ajira, biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa.






Hakuna maoni: