DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kupokea gawio pamoja na michango mbalimbali kutoka kwa taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina uwekezaji wake katika hafla ya Siku ya Gawio 2026 itakayofanyika Juni 30, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo imekusudiwa kuonesha mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kukuza uchumi wa taifa kupitia mashirika ya umma na kampuni zenye hisa za Serikali, sambamba na kuhimiza uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa mali za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Naibu Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa 2050.”
Amesema kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha taasisi za umma kuendelea kuboresha utendaji, kuongeza tija na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unawanufaisha wananchi kupitia huduma bora na mapato yanayochangia maendeleo ya taifa.
Bi. Mauki amesema Serikali imeendelea kuweka mkazo katika usimamizi madhubuti wa uwekezaji wake ili kuhakikisha mali za umma zinatoa matokeo yanayotarajiwa na kuchangia ustawi wa wananchi pamoja na ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wake, thamani ya uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma, taasisi na kampuni zenye umiliki wa hisa za Serikali imefikia takribani Sh trilioni 95, hali inayoonesha umuhimu wa kulinda na kuendeleza rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ameongeza kuwa Siku ya Gawio imekuwa sehemu muhimu ya kutathmini mchango wa taasisi na mashirika ya umma kwa Serikali kupitia gawio na michango mingine inayowasilishwa kila mwaka, huku ikitoa taswira ya mafanikio ya uwekezaji wa umma.
Aidha, amesema jukwaa hilo linaendelea kuwa daraja la kuwapatia wananchi taarifa kuhusu usimamizi wa mali za umma na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha uwekezaji wake unakuwa na tija kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Hakuna maoni: