Na Beda Msimbe, TBN, Moscow
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyepo nchini Urusi kwa ziara ya kitaifa, anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima na Chuo Kikuu cha RUDN (RUDIN) kutokana na kutambua mchango wake katika jamii ya Tanzania na dunia katika masuala yanayogusa maisha ya binadamu.
Tuzo hiyo inatolewa kama ishara ya kuthamini uongozi wake na mchango wake katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Chuo hicho kina zaidi ya wanafunzi 570 wa Kitanzania kufikia mwaka 2025, na katika kipindi cha zaidi ya miaka 65, jumla ya Watanzania 1,132 wamesoma katika chuo hicho. Kwa ujumla, RUDN kimesomesha zaidi ya wataalamu 200,000 kutoka nchi mbalimbali duniani, kikiwa na jumuiya ya wanafunzi 44,000 kutoka mataifa 160. Chuo hicho pia kimeorodheshwa nafasi ya 367 duniani kwa mujibu wa QS World University Rankings ya mwaka 2025.
Rais Dkt. Samia, aliyepokelewa jana na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi, Maxim Reshetnikov, anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin, kwa mazungumzo ya ana kwa ana yatakayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, akiwa nchini Urusi, Rais Samia—kiongozi wa pili wa Tanzania kufanya ziara rasmi nchini humo baada ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere—atashiriki Jukwaa la Uchumi la St. Petersburg. Kupitia jukwaa hilo, Tanzania itatangaza fursa za uwekezaji na kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa viongozi, wawekezaji na watunga sera wa kimataifa.
Ziara hiyo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kukuza rasilimali watu wenye ujuzi na weledi katika kusimamia miradi ya kimkakati itakayochochea ajira, viwanda na biashara, huku ikilenga kuongeza uchumi hadi kufikia dola trilioni moja na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu.
Kupitia ukurasa wake wa WhatsApp, Rais Samia alisema ziara hiyo ni muhimu katika hatua za kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
"Tutafanya mazungumzo na wenyeji wetu yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati zinazogusa maisha ya wananchi. Aidha, tutashiriki majukwaa ya biashara na uwekezaji na kutangaza fursa zilizopo nchini, pamoja na kufungua zaidi fursa za masoko kwa bidhaa za Tanzania nchini Urusi," alisema Rais Samia.

Hakuna maoni: