SAMIA AANZA ZIARA YA KITAIFA URUSI, KUPELEKA AJENDA YA UWEKEZAJI TANZANIA

Na Beda Msimbe, TBN, Moscow

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo jijini Moscow kwa ajili ya ziara ya kitaifa nchini Urusi.

Ziara hii ya kihistoria ni ya pili kufanywa na Rais wa Tanzania nchini Urusi tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo. Ziara ya kwanza ilifanywa miaka ya 1960 na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kupitia ziara hiyo, Rais Samia anaendeleza juhudi za kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na mataifa mbalimbali kwa lengo la kuongeza manufaa ya kiuchumi, uwekezaji na maendeleo ya kijamii kwa wananchi.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Rais Samia atashiriki shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria kati ya Tanzania na Urusi. Miongoni mwa shughuli hizo ni kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa St. Petersburg, ambapo anatarajiwa kuitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji na biashara.

Aidha, ziara hiyo itatoa fursa ya kujadili ushirikiano katika maendeleo ya rasilimali watu, eneo ambalo ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rais Samia aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo majira ya saa 2:25 usiku kwa saa za Moscow. Mara baada ya kuwasili alipokea heshima ya wimbo wa taifa na gwaride maalumu la mapokezi.

Katika uwanja huo, Rais Samia alipokewa na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Maxim Reshetnikov.

Kwa mujibu wa ratiba, leo asubuhi Rais Samia ataweka shada la maua katika Mnara wa Askari Asiyejulikana kabla ya kuelekea Ikulu ya Kremlin kwa mazungumzo rasmi na Rais wa Urusi, Vladimir Putin. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.