Kasulu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Simon Siro, ametoa agizo kwa wananchi waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Mkuti katika vitongoji vya Kacheri na Ligufu Relini kuondoka ndani ya eneo hilo la hifadhi ifikapo Julai 30, 2026 na kuhamia katika eneo walilotengewa ndani ya Kijiji cha Zeze.
Agizo hilo limetolewa Juni 20, 2026 wakati wa ziara ya Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kigoma na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kasulu, iliyofanyika kwa kushirikiana na Kamanda Mhifadhi wa Kanda ya Magharibi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa lengo la kutekeleza mpango wa kuwaondoa wavamizi ndani ya hifadhi hiyo.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Siro alikagua shule iliyotengwa kwa ajili ya wanafunzi watakaohamishwa kutoka eneo la hifadhi na kueleza kuridhishwa na maandalizi yaliyofanyika. Pia alifanya mikutano na wananchi wa vitongoji husika na kusisitiza kuwa muda uliotolewa unapaswa kutumika kukamilisha uhamaji kwa hiari.
Alisema kuwa Serikali imeweka mazingira stahiki ya makazi mapya kwa wananchi hao na kuwataka viongozi wa Wilaya ya Kasulu, Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na TFS kuhakikisha maandalizi yote yaliyosalia yanakamilika kabla ya Julai 30, 2026 ili kuepusha malalamiko wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Mhe. Siro alionya kuwa kuanzia Agosti 1, 2026, mtu yeyote atakayebainika kuendelea kuishi ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mkuti ataondolewa kwa nguvu kupitia operesheni maalumu ya Serikali.
Aidha, aliwataka wananchi hao kuwa makini na matapeli wanaowatoza fedha kwa madai ya kuwasaidia kubaki ndani ya hifadhi, akisisitiza kuwa hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya Serikali kuhusu uhifadhi wa eneo hilo.






Hakuna maoni: