TAKUKURU TEMEKE YAREJESHA SH. MILIONI 87, YAFIKISHA MAHAKAMANI WATUHUMIWA 12 WA UBADHIRIFU

Na Mwandishi Wetu, 

Temeke.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kusimamia urejeshwaji wa Shilingi milioni 87 zilizokuwa zimepotea kutokana na ubadhirifu wa fedha za umma katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Akizungumza katika taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Fransis Luena, alisema hatua hiyo imepatikana baada ya uchunguzi uliofanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuhusu tuhuma za wizi na ubadhirifu wa fedha kiasi cha Shilingi 169.6 milioni maarufu kama fedha za bakaa.

Alisema watuhumiwa 12, wakiwemo watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni pamoja na wafanyabiashara watatu, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa mbalimbali yakiwemo kuendesha genge la uhalifu, ubadhirifu, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara.

Kwa mujibu wa Luena, washtakiwa watatu ambao ni Juvenalis Babilas Mauna, Josephat Mutembei na Hamis Kashinje Manfred walikiri makosa yao kupitia utaratibu wa makubaliano ya kisheria (plea bargain), ambapo walirejesha jumla ya Shilingi milioni 87 na kulipa faini ya Shilingi milioni 3.5.

“Juvenalis Mauna amerejesha Shilingi milioni 27 na kulipa faini ya Shilingi milioni mbili, Hamis Kashinje Manfred amerejesha Shilingi milioni 40 na kulipa faini ya Shilingi milioni 1.5, huku Josephat Mutembei akirejesha Shilingi milioni 20,” alisema Luena.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Temeke ilifuatilia matumizi ya zaidi ya Shilingi bilioni 6.5 zilizotengwa kwa utekelezaji wa miradi saba ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na ujenzi katika Manispaa za Temeke na Kigamboni, huku ikibaini changamoto katika miradi miwili ambazo zilifanyiwa maboresho na kukamilika kwa wakati.

Aidha, taasisi hiyo ilitoa elimu ya kupambana na rushwa kwa wananchi 20,804 kupitia mikutano, semina, maonesho na vipindi vya redio, pamoja na kuimarisha klabu 30 za wapinga rushwa katika shule na vyuo.

Luena alisema TAKUKURU pia ilifanikiwa kuokoa na kurejesha Shilingi 370,000 kwa madereva 40 wa bajaji wa kituo cha Kibada, Kigamboni, waliokuwa wametozwa fedha isivyo halali kwa madai ya kulipia stika za maegesho.

Kwa upande wa malalamiko, alisema taasisi hiyo ilipokea malalamiko 68 katika robo ya Januari hadi Machi 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.7 ikilinganishwa na robo iliyopita, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa imani ya wananchi katika kuripoti vitendo vya rushwa.

Aliongeza kuwa asilimia 76.5 ya malalamiko hayo yanahusu rushwa na yanaendelea kufanyiwa uchunguzi, huku kesi moja mpya ikifunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya kesi tano kuendelea kusikilizwa.

Luena aliwahimiza wananchi wa Temeke na Kigamboni kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia ofisi za taasisi hiyo au kupiga simu ya bure 113 inayopatikana saa zote.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.