TANZANIA NA CANADA KUSHIRIKIANA KWENYE UTAFITI WA KINA WA MADINI NCHINI

Dodoma

Tanzania na Canada zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya utafiti wa kina wa madini, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia, kuhamasisha uwekezaji na kuendeleza Sekta ya Madini nchini.

Hayo yameelezwa leo Juni 16, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati wa kikao chake na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Emily Burns, kilicholenga kujadili namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika eneo la utafiti wa madini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mavunde amesema Tanzania hivi sasa inajipanga kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha na badala yake kuwa na uchimbaji unaoongozwa na taarifa muhimu za kijiolojia,huku akisisitiza kuwa mkakati uliopo ni kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa Tanzania na Canada zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na kwamba ameridhishwa na dhamira iliyooneshwa na Serikali ya Canada ya kushirikiana na Tanzania katika miradi ya kimkakati ya utafiti wa kina wa madini.

Aidha, amesema tafiti za kina zitasaidia kuondoa changamoto ya uchimbaji wa kubahatisha ambayo imekuwa ikiwasababishia wachimbaji wadogo kupoteza muda, mitaji na rasilimali nyingine kutokana na kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo yasiyokuwa na taarifa za kutosha za kijiolojia.

Mhe. Mavunde ameielekeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuainisha maeneo ya kimkakati yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa ushirikiano huo, huku akisisitiza kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano wote unaohitajika ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Emily Burns, amesema Serikali ya Canada imevutiwa na maono ya *Mining Vision 2030* pamoja na kaulimbiu ya *“Madini ni Maisha na Utajiri”*, na kueleza kuwa nchi hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo utafiti wa kina wa madini kwa kutumia teknolojia ya uchunguzi wa angani kupitia ndege maalum.

Naye Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuanza kwa kufanya tafiti za kina katika Block Na. 1 iliyopo Kanda ya Ziwa na Block Na. 5 iliyopo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, maeneo ambayo ni miongoni mwa vipaumbele vya taasisi hiyo katika mwaka wa fedha ujao.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia, kuimarisha uwekezaji na kuchochea ukuaji endelevu wa Sekta ya Madini, sambamba na kuiwezesha Tanzania kufikia lengo la kuongeza eneo la utafiti wa kina kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.