TANZANIA YAJIPANGA KUWA NGOME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI AFRIKA

Dar es Salaam, 

Na Mwandishi Wetu. 

Tanzania imeendelea kuchukua hatua muhimu katika kuimarisha usalama na ulinzi wa taarifa binafsi katika enzi ya ukuaji wa kasi wa teknolojia za kidijitali, huku Serikali ikisisitiza kuwa ulinzi wa faragha ya wananchi ni msingi muhimu wa kujenga uchumi imara wa kidijitali unaoaminika na jumuishi kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.

Kongamano la kwanza la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi limefunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam likiwa na kaulimbiu isemayo “Faragha ya data kama nguzo kuu: Kulinda mustakabali wa uchumi wa kidijitali jumuishi kuelekea Dira ya 2050” (Data privacy as the pillar: securing inclusive digital future towards Vision 2050), likilenga kuwaleta pamoja wadau kujadili mustakabali wa ulinzi wa taarifa binafsi nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Switbert Zacharia Mkama, amesema taarifa binafsi ni nyenzo muhimu inayomtambulisha mtu, hivyo ni lazima ilindwe kikamilifu ili kulinda utu, haki na usalama wa wananchi katika mazingira ya kidijitali.

Amesema kwa kuzingatia kasi ya mabadiliko ya teknolojia, hususan ukuaji wa huduma za mtandaoni na mifumo ya kidijitali, Serikali iliona umuhimu wa kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mwaka 2022 ili kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi, elimu na utekelezaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi nchini.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa uchumi wa kidijitali hauwezi kujengwa kwa teknolojia pekee, bali unahitaji kiwango kikubwa cha uaminifu na usalama wa taarifa zinazochakatwa na mifumo mbalimbali ya kidijitali, akisisitiza kuwa huduma za serikali na sekta binafsi zinapohamia kidijitali, ulinzi wa taarifa za wananchi ni jambo lisiloepukika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema kongamano hilo ni la kihistoria kwani ni la kwanza kufanyika tangu kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mwaka 2022, likitoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kupanga mikakati ya baadaye.

Amesema Tanzania inashuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali, hali inayoongeza kasi ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa, hivyo kuhitaji mifumo thabiti ya ulinzi wa taarifa hizo ili kulinda faragha ya wananchi.

Dkt. Mkilia amesisitiza kuwa faragha ya taarifa binafsi si kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali bali ni msingi muhimu unaojenga imani na usalama, akibainisha kuwa bila ulinzi madhubuti wa taarifa, ukuaji wa uchumi wa kidijitali hauwezi kuwa endelevu.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume hiyo, Dkt. Adadi Mohammed Rajabu, amesema kufanyika kwa kongamano hilo ni hatua muhimu kwa Tanzania katika kuimarisha misingi ya uaminifu, haki na uwajibikaji, jambo litakalosaidia kuongeza imani ya wananchi, wadau na wawekezaji katika mifumo ya kidijitali.

Amesema mabadiliko ya teknolojia, hususan akili mnemba (AI) na huduma za mtandaoni, yamefungua fursa kubwa za ubunifu na uwekezaji, lakini yameleta pia hitaji la kuimarisha zaidi ulinzi wa taarifa binafsi bila kuzuia ubunifu huo.

Dkt. Rajabu amesisitiza kuwa maendeleo ya kidijitali yanapaswa kwenda sambamba na heshima ya utu wa binadamu na misingi ya usalama wa taarifa, akieleza kuwa Tanzania inalenga kuwa kitovu cha ulinzi wa taarifa binafsi kikanda na kimataifa.

Kongamano hilo linatarajiwa kuendelea kwa siku mbili kuanzia leo Juni 29 hadi julai 01,2026 majadiliano kutoka kwa wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya TEHAMA, sheria na sekta binafsi, likilenga kuibua suluhisho na mikakati ya kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi nchini. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.