Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO
Arusha. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia Maonesho ya Karibu-KiliFair 2026 yanayoendelea jijini Arusha kutangaza vivutio vya utalii wa misitu na ikolojia vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza idadi ya watalii na kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii wa asili.
Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Zuberi Mabie, amesema ushiriki wa wakala huo katika maonesho hayo unalenga kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo kwenye maeneo yanayosimamiwa na TFS, kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya utalii na kufungua fursa mpya za uwekezaji.
Amesema maonesho ya Karibu-KiliFair yameendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi, huku yakitoa nafasi ya kutangaza bidhaa na huduma zinazochangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Tunashiriki katika maonesho haya kwa lengo la kuhakikisha watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali wanapata fursa ya kufahamu vivutio na shughuli za utalii zinazopatikana katika maeneo yanayosimamiwa na TFS, hususan Kanda ya Kaskazini ambayo imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya asili,” amesema Mabie.
Ametaja baadhi ya vivutio vinavyotangazwa kupitia maonesho hayo kuwa ni Ziwa Duluti, Mlima Hanang, Maporomoko ya Maji ya Napuru yaliyopo Wilaya ya Meru pamoja na Shamba la Miti Meru, ambalo limeendelea kuwa kivutio muhimu kwa watalii wanaopenda utalii wa mazingira.
Mabie amesema TFS pia imeandaa matukio mbalimbali yatakayowapa wananchi na wageni fursa ya kutembelea na kujionea vivutio hivyo, yakiwemo mashindano ya West Kilimanjaro Tour Challenge na tukio la kupanda Mlima Hanang yatakayofanyika Juni 21, 2026, pamoja na ziara maalumu ya kutembelea Maporomoko ya Maji ya Napuru itakayofanyika Agosti 29 hadi 30, 2026.
Ameongeza kuwa utalii wa misitu una mchango mkubwa katika uhifadhi wa rasilimali za asili, huku ukiendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Awali, Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi, amesema Karibu-KiliFair imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika kwa kuongeza idadi ya watalii, kuvutia wawekezaji wapya na kufungua masoko mapya ya huduma na bidhaa za utalii.
Amesema maonesho hayo si tukio la kawaida bali ni uwekezaji wa kimkakati unaochochea ukuaji wa sekta ya utalii na kutoa fursa kwa taasisi mbalimbali, ikiwemo TFS, kuonesha mchango wake katika maendeleo ya utalii wa ikolojia na uhifadhi wa rasilimali za asili.

Hakuna maoni: