TMA YAPOKEA WATAALAMU WA DENMARK KUIMARISHA MTANDAO WA UANGAZI WA HALI YA HEWA



Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea ujumbe wa wataalamu kutoka Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI) chini ya Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF), kwa lengo la kuimarisha mtandao wa vituo vya hali ya hewa nchini na kufikia viwango vya Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi wa Hali ya Hewa (GBON).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ziara hiyo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema ujio wa wataalamu hao unaonesha dhamira ya pamoja ya kuendelea kuimarisha uwezo wa TMA katika shughuli za uangazi wa hali ya hewa.

Amesema uwekezaji unaofanywa kupitia mradi wa SOFF unalenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kutimiza viwango vya GBON huku ikiboresha ubora na usahihi wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa jamii, taifa, kanda na kimataifa.

“Lengo letu ni kuhakikisha TMA inaendelea kutimiza viwango vya GBON kwa muda mrefu huku ikiboresha ubora wa huduma za hali ya hewa,” amesema Dkt. Chang’a.

Kwa mujibu wa TMA, ziara hiyo ya kitaalamu itahusisha tathmini ya uwezo wa mamlaka katika maeneo mbalimbali ikiwemo mfumo wa ubadilishanaji wa taarifa za hali ya hewa kimataifa, matengenezo ya vifaa, ujenzi wa uwezo kwa wataalamu, huduma za uhakiki wa vifaa pamoja na uendeshaji wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa vya ardhini na anga la juu.

Meneja wa Mradi kutoka DMI, Dkt. Sebastian Hornum, amesema ziara hiyo inatoa fursa muhimu kwa wataalamu wa pande zote mbili kushirikiana katika kubaini mbinu za kuimarisha uwezo wa kiufundi na kufikia viwango vya kimataifa vya uangazi wa hali ya hewa.

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Uratibu wa Mradi wa SOFF kutoka UNDP, Dkt. Abbas Kitogo, amesema mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yanaonyesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya TMA, DMI na UNDP.

Amesema taasisi hizo zitaendelea kushirikiana kuhakikisha mradi wa SOFF unatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Ziara hiyo pia itahusisha kutembelea vituo vya uangazi wa hali ya hewa vilivyopo Dodoma na Dar es Salaam ambavyo vimejumuishwa katika mtandao wa GBON, kwa ajili ya kutathmini hali ya uendeshaji na kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.