Dodoma.
Tume ya Madini imeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sekta ya madini katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu rasilimali madini na fursa zinazotokana na sekta hiyo.
Maonesho hayo yaliyoanza leo Juni 16, 2026 yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026, yakikutanisha taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kuonesha huduma wanazotoa kwa wananchi chini ya kaulimbiu isemayo, “Kuchochea Uwajibikaji kwa Huduma Endelevu.”
Kupitia banda lake, Tume ya Madini inatoa elimu kuhusu aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini, mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa taifa, pamoja na fursa za uwekezaji, ajira na ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Aidha, wananchi wanaotembelea banda la Tume wanapata fursa ya kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi kwa wadau wa sekta ya madini, sambamba na kupata ufafanuzi kuhusu taratibu na miongozo inayosimamia shughuli za madini nchini.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho Juni 17, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.
Wananchi wamehimizwa kutembelea mabanda mbalimbali ili kujionea huduma zinazotolewa na taasisi za umma na kupata elimu itakayowawezesha kunufaika na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo sekta ya madini.





Hakuna maoni: