Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani kupitia Upendo Media, limetangaza kuwa Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu 2026 litafanyika Juni 13, 2026 katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam. Tamasha hilo linatarajiwa kukutanisha zaidi ya vijana 35,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa DMP, Mchungaji Wilbroad Mastai, alisema lengo kuu la tamasha hilo ni kuwajengea vijana mtazamo chanya utakaowasaidia kuishi maisha yenye maadili mema mbele za Mungu na jamii. Alieleza kuwa tamasha hilo linafanyika kwa mara ya 13 tangu lilipoanzishwa mwaka 2014 katika Usharika wa KKKT Kijitonyama, Dar es Salaam.
Aidha, imeelezwa kuwa pamoja na washiriki kutoka Tanzania, vijana kutoka Botswana tayari wamewasili nchini kwa ajili ya kujifunza namna tamasha hilo linavyoandaliwa ili waweze kuanzisha utaratibu kama huo katika nchi yao.
Kwa mujibu wa waandaaji, tamasha hilo linalenga kuunganisha watu wa dini na itikadi mbalimbali ili kujenga taifa lenye misingi ya nidhamu, uwajibikaji, uzalendo na kujituma. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Be the Star”, ikihamasisha vijana kuwa mfano bora wa maadili katika jamii.
Katika kilele cha tamasha hilo, waimbaji mbalimbali wa muziki wa injili watatumbuiza akiwemo Rose Mhando, Boaz Danken, Agape Gospel Band, Neema Gospel Kwaya, Hyper Squad pamoja na kwaya mbalimbali za KKKT. Tamasha hilo litafunguliwa na Askofu Alex Malasusa huku Neno la Mungu likitarajiwa kuhubiriwa na Askofu Jackson Sostenes.
Waandaaji wamesema maandalizi yote muhimu yamekamilika, yakiwemo huduma za usalama, chakula, maji na huduma ya kwanza ili kuhakikisha washiriki wanapata mazingira salama na bora wakati wote wa tamasha.
Pia wametoa wito kwa wazazi na walezi kuwaruhusu vijana kushiriki tukio hilo ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka wakati wa likizo. Tamasha litaanza saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, huku kiingilio kikiwa shilingi 5,000 na tiketi zikiwa tayari zinapatikana.



Hakuna maoni: