VIUATILIFU, MBEGU ASILI ZANUFAISHA WAKULIMA

Na Mwandishi Wetu.

MATUMIZI ya mbegu na viuatilifu vya asili yametajwa kuhamasisha kilimo ikolojia kwa wanakijiji cha Ekenywa mkoani Arusha.

Matumizi hayo yametokana na elimu iliyotolewa na Shirika la Shirika lisilo la Kiserikali la Utafiti, Ushauri wa Kitaalamu na Miradi ya Maendeleo na Jamii (RECODA) na Island of Peace (IDP) kwa wakulima wa kijiji hicho.

Mkulima Loma Lotaswariake wa Kikundi cha Afya kijiji cha Ekenywa kata ya Elitrumet alisema mashirika hayo yamemuwezesha kujua kilimo hai kinahitaji uhifadhi wa ardhi, ili wasiharibu viumbe ambavyo vinameng'enya udongo.

"Tumefundishwa mbinu za kutengeneza viuatilufu vya asili, badala ya kutumia vya sumu ambavyo vinaathiri afya zetu na wadudu pia," alisema

Lotaswariake alisema matumizi ya viuatilifu vya asili vimewezesha mazao yao kutoshambuliwa na wadudu waharihifu, akitolea mfano matumizi ya muarobaini.

"Kwa sasa hatutumii viuatilifu venye kemikali za sumu kwenye kilimo, hali ambayo inaboresha afya zetu, lakini soko la uhakika la mazao yetu," alisema.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Afya, Lucas Lekuye alisema kilimo ikolojia kimejuwezesha kuongeza uzalishaji, kutoka gunia 12 hadi 20 kwa heka ya mahindi.

Alisema wanakikundi wapo 30 na 21 ni wanawake jambo ambalo linaonesha matumaini.

Lekuye alisema pia kilimo hicho kina mhakikishia soko la mazao yake, hivyo kuwa na kipato cha uhakika, huku akiomba Serikali na wadau wengine kuwawezesha kupata maji kwa msimu mzima.

"Elimu niliyopatiwa kuhusu kilimo ikolojia, imenikomboa sana, naomba serikali iwekeze kwenye kilimo hiki kina faida kwa mkulima, ardhi na mlaji," alisema.

Martha Samweli wa Kikundi cha Namaiyani alisema kikundi chao kina wanachama 41 ambapo wanawake ni 35 na wanaume sita na kwamba elimu ambayo wamepata imeweza kumkomboa kiuchumi na afya.

"Tumejifunza kilimo cha mbogamboga, migomba, viazi lishe, mihogo, kupiga dawa za asili shambani na kuweka akiba, hali ambayo inatuwezesha kuendesha maisha yao," alisema.

Martha alisema pia wanafuga kuku na nguruwe ambao wanauaza na kujiongezea kipato.

"RECODA na IDP wametufaa kwani kwa tumeweza kuanzisha vikundi vingine kwenye kijiji jirani," alisema.

 Aidha, alisema ujio wa mashirika hayo yameboresha afya yake, kwani awali alikuwa anakula vyakula vyenye sumu ambavyo vilikuwa na athari kwenye afya yake.

Alisema kilimo ikolojia kina gharama ndogo na faida nyingi, kwa kuwa soko ni la uhakika.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ekenywa, Wilson Piniel alisema RECODA na IDP wameleta mageuzi chanya kijijini hapo, jambo ambalo linamrahisishia kuongoza.

Alisema uongozi wake utahakikisha miradi hiyo inaendelea, kwani ina faida zaidi kwa wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa RECODA, Josephine Ng'ang'a alisema kinachoonekana kwenye Mradi wa Kilimo Endelevu ni matokeo ya Mfumo wa Ugani wa Jitihada za Shirikishi za Kuleta Mageuzi ya Kilimo Vijijini (RIPAT), ambao unawaongoza katika utekelezaji wa miradi yao.

Alisema mradi huo umehusisha vijiji 10 ambapo kila kijiji kiliunda vikundi viwili ambavyo vinatekeleza kilimo kwa mbinu za kiikolojia.

Ng'ang'a alisema vikundi vya Afya na Namaiyani vimeonesha matokeo mazuri jambo ambalo linapaswa kuigwa na maeneo mengine.

Alisema mradi huo umeweza kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kurutubisha ardhi.

Meneja wa Miradi kutoka IDP, Ermelinda Temba alisema matokeo chanya yanayooneka kwenye vijiji ndio tamanio la shirika lao kwa kushirikiana na wadau wa kilimo ikolojia.

Temba alisema kupitia Mradi wa Agro Kilimo mkoani Arusha wameona namna RIPAT imeleta mabadiliko chanya ikiwemo kuzalisha wakulima vichocheo kwenye kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa nguruwe na kuku.

Alisema IDP inashirikiana na vituo vya kilimo ikolojia kama RECODA, SJS Mwanga, Shirika la Kuendeleza Kilimo (SAT), MFEC, PPIZ na Bihawana.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.